Pages

Thursday, May 16, 2013

DC BUNDA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI

 

 MKUU wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Mirumbe, amewakutanisha wakazi wa Kata ya Mikomariro wilayani Bunda na Silolisimba wilayani Butiama wanaogombania mipaka ya ardhi.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jana katika Kijiji cha Mikomariro, Mirumbe alisema ameamua kuitisha kikao hicho kwa ajili ya kuwakutanisha viongozi wa serikali za vijiji na viongozi wa kamati za ulinzi na usalama, ili kuzungumzia suala hilo ambalo limekuwa likileta hali ya kutoelewana.

Wakichangia maoni katika kikao hicho baadhi ya wananchi walidai mgogoro huo ni wa muda mrefu na kwamba licha ya kusuluhishwa mara nyingi mwafaka haujapatikana.

Mmoja wa wananchi, Alfred Mniko, alisema mwaka juzi walikaa kikao kati ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Musoma na walipewa maelekezo kuhusu mipaka hiyo, lakini wenzao wa Mikomariro hawakuridhika.

Naye Marabha Mwita alidai kuwa mwaka 1990 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali mstaafu Issa Machibya alifika katika eneo hilo akawapa ramani ya mipaka inayogombewa na kutaka kila upande uheshimu mipaka hiyo lakini bado vurugu zimekuwa zikijitokeza.

“Mgogoro huu unaendeshwa kisiasa, lakini pia wataalamu wamechangia, mfano wakurugenzi waliagizwa siku hiyo na mkuu wa mkoa waweke maboya katika mipaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo, lakini hadi leo jambo hilo halijatekelezwa,’’ alisema Juma Werema.

Akihitimisha kikao hicho, mkuu huyo wa wilaya alisema haoni sababu ya wananchi hao kugombania mipaka na kwamba wanaofanya uharifu wa kuchomea wenzao nyumba kwa kisingizio cha mipaka ya ardhi waache mara moja kwani hilo ni kosa la jinai.

Aliwaagiza wenyeviti wa maeneo hayo kuitisha mikutano ili waweze kukaa na wananchi wao kwa ajili ya kuzuia vitendo viovu wakati serikali ikishughulikia suala hilo.

No comments:

Post a Comment