Pages

Saturday, May 18, 2013

ZITO AWASHA MOTO BUNGENI

 

 WABUNGE wa CHADEMA; Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na John Mnyika (Ubungo), wamewachochea wabunge wenzao wasihudhurie semina iliyoandaliwa leo na Wizara ya Nishati na Madini.

Sababu waliyoitoa wabunge hao juu ya ushawishi huo ni kuwa serikali imeanza ugawaji wa vitalu vipya vya mafuta na gesi kwenye bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.

Hata hivyo, hatua hiyo imeonekana kuwagawa wabunge, ambapo baadhi wamepinga na wengine kuunga mkono.

Kupitia taarifa zao kwa vyombo vya habari walizozituma kwa nyakati tofauti, Zitto na Mnyika wamepinga uamuzi wa serikali wa kuanza mzunguko wa nne wa ugawaji wa leseni za utafutaji na ugunduzi wa gesi nchini.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto ameonesha kushangazwa na uamuzi huo wa serikali, kwani Tanzania bado haijawa na sera ya gesi asilia na kwamba ndiyo kwanza wabunge wamepewa rasimu ya sera hiyo kwa ajili ya kutoa maoni yao.

“Kesho Jumamosi wabunge tumealikwa kwenye semina kuhusu sera ya gesi asilia. Tumegawiwa tayari nakala zetu, tena zipo kwenye lugha ya kimombo,” alisema Zitto na kuongeza;

“Jambo la kushangaza ni kwamba wakati sera ya gesi asilia ipo kwenye rasimu na ndiyo kwanza wabunge tumeletewa kutoa maoni, serikali tayari imetangaza tena kugawa vitalu vya mafuta na gesi kwenye bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.”

Pia katika taarifa hiyo Zitto ameelezea kushangazwa na hatua hiyo ya serikali ambayo alisema inakwenda kinyume cha maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozuia ugawaji mpya wa vitalu hadi sera ya gesi asilia na sheria ya gesi vikamilike.

“Haraka hii ya serikali kugawa vitalu bila sera wala sheria inatoka wapi? Nitashangaa sana wabunge kukimbilia posho za semina hii na kuhalalisha maamuzi yasiyozingatia maslahi ya taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza Zitto.

Zitto amewataka wabunge na wananchi kuupinga uamuzi huo wa serikali.

“Uamuzi wa kugawa vitalu vipya bila kwanza kuwepo kwa sera na sheria mpya unapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Tafuta mbunge wako, mwambie asikubali maamuzi haya ya serikali. Tumalize kwanza sera na sheria ndiyo tugawe vitalu vipya. Gesi sio viazi, haiozi,” imesisitiza taarifa hiyo.

Naye Mnyika amesema kuwa si sahihi kwa serikali kuanza kutoa leseni mpya za utafutaji na ugunduzi wa gesi nchini wakati taifa likiwa bado linaendelea na mchakato wa katiba mpya.

“Taifa letu lipo kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya huku kukiwa na kumbukumbu chungu za miaka zaidi ya 20 ya kupata hasara kubwa baada ya kufungua mianya ya ufisadi na unyonywaji katika sekta ya uchimbaji madini na rasilimali zingine muhimu,” ilisema taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Taarifa hiyo inapendekeza kuwa ingekuwa vema kwa serikali kusubiri kwanza kukamilika kwa mchakato wa kupata katiba mpya ili kuhakikisha kuwa udhaifu wa kikatiba, kisera, kisheria, kiuongozi na kitaasisi umerekebishwa.

“Hivyo, badala ya kukimbilia kutangaza mzunguko mwingine huku tayari taifa likiwa kwenye lindi la ufisadi na unyonyaji kupitia mikataba iliyotangulia ya gesi asili; nguvu za wananchi zielekezwe katika kutaka katiba mpya kuwa na vifungu vitakavyolinda rasilimali muhimu kama mafuta, gesi madini na mali asili nyingine,” imesisitiza taarifa hiyo.

Hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetoa taarifa ya kuzinduliwa kwa mzunguko wa nne wa utoaji leseni za utafiti na ugunduzi wa gesi asilia nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari, na tovuti ya TPDC ni kwamba utoaji leseni za utafiti na uzinduzi huo utaanza mwezi Oktoba, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, leseni zitakazotolewa zitahusisha utafiti katika Ziwa Tanganyika lililopo magharibi mwa Tanzania, na ndani ya kina kirefu cha maji ya Bahari ya Hindi kwa upande wa mashariki na kusini mwa bahari hiyo.

Itakumbukwa kwamba hapo awali wizara ilitangaza kutokuingia mikataba yoyote ya utafiti na uvumbuzi wa gesi asilia hadi pale sera ya mafuta na gesi itakapokuwa tayari.

Msimamo wa CHADEMA kuhusu sekta ya mafuta na gesi uko wazi ambapo inataka kwanza kuandaliwa kwa sera na sheria ya mafuta na gesi kabla ya kuingia mikataba mipya ya utafutaji na ugunduzi wa nishati hizo.

Baadhi ya wabunge wamelidokeza Tanzania Daima kuwa kutohudhuria semina hiyo ni kujikosesha fursa ya kujua kitakachowasilishwa na serikali.

Walibainisha kuwa wasipohudhuria semina hiyo hawatakuwa na uwanja mpana wa kupinga kile wanachokiona si sawa.

Waziri Muhongo anena

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema Tanzania inatumia sheria ya gesi asilia na mafuta ya mwaka 1980.

“Watu waache kupotosha..., si kweli kuwapo maamuzi ya Bunge ya kutogawa vitalu vipya vya utafutaji wa gesi asilia na mafuta bali kinachofanyika ni kuiboresha sera na sheria ya gesi asilia ili kuitengenisha na mafuta,” alisema.

Alisema kuwa utafutaji huo haukuanza leo na kwamba anayegundua ndiye anatafuta sana.

Profesa alifafanua kuwa kwa sasa wanafanya maboresho ya kulijenga upya Shirika la Mafuta (TPDC) lililoanzishwa mwaka 1969.

“Hawa Watanzania wanaotoa taarifa za uongo kwenye mitandano na kutaka kupotosha watu, wanaikosesha nchi maendeleo. Maana hayo makampuni ya mafuta wanayoyapiga vita ndiyo hayo yanatafuta mafuta Msumbiji na Kenya, kwanini sisi tukatae?” alihoji.

Alisema kuwa kama nchi isingekuwa na sera ya gesi na mafuta hata hao wawekezaji wasingekubali kuwekeza kwenye nchi ambayo haina sheria.

Waziri Muhongo alisema kuwa leo watafanya semina kwa wabunge wote mjini hapa kuhusu sera hiyo ya gesi, na hivyo kuwataka wote wenye dukuduku walete hoja zao wapate ufafanuzi.

No comments:

Post a Comment