Pages

Wednesday, May 15, 2013

Manusura aliishi kwa biskuti, maji

Manusura wa jengo lililoporomoka nchini Bangladesh, Reshma Begum akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa jeshi kwenye hospitali ya jeshi mjini Dhaka, Bangladesh  baada ya kuokolewa na kupatiwa huduma ya kwanza, ambapo alieleza namna alivyonusurika. Picha na AFP 

 

Kwa ufupi

  • Japan mwaka 2004: Mtoto mwenye umri wa miaka miwili aliokolewa akiwa hai baada ya siku nne, ndani ya gari lililokuwa limezikwa ardhini.

  • Iran mwaka 2004: Mwanamke aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 90 aliokolewa akiwa hai baada ya siku nane za kufukiwa na mabaki ya nyumba yake iliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi.

  • Korea Kusini mwaka 1995: Mwanamke aliyekuwa amefukiwa na mabaki jengo la duka kwa siku 16, aliokolewa akiwa hai.

HABARI :

  Msichana aliyenusurika baada ya kuishi kwa siku 17 chini ya kifusi cha ghorofa lililoporomoka mjini Dhaka, Bangladesh, amesema biskuti alizonunua kwa ajili ya kifungua kinywa akiwa kazini ndizo zilimnusuru kufa kwa njaa.

Reshma Begum aliishangaza dunia baada ya kuokolewa chini ya kifusi cha jengo hilo, lililoporomoka Aprili 24, mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.watu zaidi ya 2,500 waliokolewa kati ya watu zaidi ya 3,000 ambao walikuwa wakifanya kazi ndani ya jengo hilo la ghorofa nane.

Msichana huyo ambaye hakuwa na majeraha ya kuhatarisha maisha yake, alisimulia mkasa wake kwamba aliishi kwa kula biskuti na kunywa maji ya chupa yaliyodondoka kwenye eneo lake, bila kufahamu yalikotoka.

Reshma (19) alisema siku ya ajali hiyo, aliamka asubuhi kuwahi kazini bila kupata kifungua kinywa ambapo akiwa njiani alinunua mabunda madogo manne ya biskuti ambazo angekula kabla ya kuanza kazi.

Msichana huyo aliwasimulia mkasa huo wafanyakazi wa hospitali na waokoaji kuwa aliishi kwa kula biskuti na kunywa maji ya chupa, akiwa kwenye shimo lililokuwa na nafasi ya kumuwezesha kutembea.

Maji ya chupa aliyokuwa akitumia Reshma ni miongoni mwa yaliyokuwa yakidondoshwa na waokoaji, kwenye kila shimo la eneo la tukio.

Kwa mujibu wa taarifa, waokoaji walipewa maelekezo ya kudondosha chupa za maji katika kila shimo watakaloona, kwa dhamira ya kubahatisha huwenda chini ya shimo kuna binadamu walio hai na maji hayo yalilenga kuwasaidia wakati juhudi za uokoaji zikiendelea.

Reshma ambaye anaishi peke yake katika chumba cha kupanga kwenye kitongoji cha Savar, alisema wakati jengo hilo la ghorofa nane lilipokuwa likiaguka alikuwa ghorofa ya tatu.

Alisema aliweza kushuka hadi ghorofa ya pili ambako alinasa kwenye shimo kubwa. Alisema shimo hilo lilikuwa kubwa kumuwezesha kutembea na kulikuwa na hewa ya kutosha.

Reshma alisema alipokwama kwenye shimo hilo pia nywele zake zilibanwa na maporomoko ya mabaki ya jengo, ambapo alilazimika kuzivuta hadi zikakatika ili awe huru.

Alisema licha ya kupiga kelele ya kuomba msaada hakuweza kufanikiwa, na kwamba giza ndani ya shimo hilo lilimfanya asijue usiku wala mchana.

No comments:

Post a Comment