Pages

Friday, May 17, 2013

GARI MOSHI LA MWAKYEMBE KUBINAFSISHWA


BAADA ya Serikali kubuni na kufanikiwa kuanzisha na kuendesha usafiri wa treni jijini Dar es Salaam, sasa inajipanga kubinafsisha usafiri huo unaosaidia kupunguza msongamano. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alisema hayo bungeni jana, wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Alisema Serikali inakamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji na mwendeshaji wa huduma hiyo jijini humo.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), ndiyo itakayokamilisha mchakato wa kumpata mwekezaji na mwendeshaji wa huduma hiyo, atakayetumia miundombinu ya reli iliyopo na vichwa vya treni na mabehewa maalumu ya usafiri katika miji.

Dk Mwakyembe alisema mwitikio wa wananchi kutumia huduma ya treni ya abiria, umekuwa mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma yenyewe, hususan nyakati za mahitaji makubwa ya usafiri.

Wingi wa abiria Kwa sasa kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, treni hiyo ya jijini Dar es Salaam, inabeba watu 14,000 kwa kila siku, sawa na zaidi ya daladala 467 zenye uwezo wa kubeba abiria 30 kila siku.

“Kwa upande wa Tazara, wastani wa idadi ya abiria wanaosafiri kwa treni kwa siku, umefikia 9,000 baada ya kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa mengine saba na kichwa kimoja cha treni na kuanza kutumika rasmi Mei 9, 2013.

“Aidha, kwa upande wa TRL, wastani wa abiria wanaosafiri kwa siku ni 5,000,” aliongeza Dk Mwakyembe akizungumzia usafiri huo ulioanza Oktoba mwaka jana, kati ya Stesheni na Ubungo Maziwa na kati ya Tazara na Mwakanga.

Faida, changamoto Alisema kuanzishwa kwa usafiri huo wa treni jijini Dar es Salaam, kumesaidia kumepunguza idadi ya magari barabarani.

“Kuanza kwa usafiri huu, kumeshawishi baadhi ya wananchi waliokuwa wanatumia magari binafsi kuja katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kuanza kutumia usafiri wa treni,” alisema Dk Mwakyembe.

Alizitaja baadhi ya faida zingine zinazotokana na usafiri huo, kuwa ni kupungua kwa matumizi ya mafuta, muda unaotumika barabarani na hivyo kusaidia wananchi kufika kwa wakati katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Alisema Wizara inaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizojitokeza, zikiwamo za kutokuwa na mfumo thabiti wa kukusanya mapato, uchakavu wa miundombinu na uhaba wa injini na mabehewa.

Kuhusu kuongeza huduma za usafiri huo, alisema Wizara imeunda Kamati Maalumu chini ya uenyekiti wa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, ili kuchambua, kuainisha na kushauri mipango na mikakati ya kuboresha na kupanua usafiri huo.

Ruti mpya “Pia Wizara inaangalia uwezekano wa kuanzisha huduma maalumu ya treni kati ya Stesheni ya Dar es Salaam na Gongo la Mboto kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaopita kwenda Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere,” alisema Dk Mwakyembe.

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilishauri kuwa ili mradi huo ufanye kazi kwa ufanisi na kuondokana na hasara, Serikali iharakishe kununua angalau treni mbili za kisasa na maalumu kwa safari fupi, ambazo gharama yake ni Sh bilioni 8 kila moja

No comments:

Post a Comment