Pages

Saturday, May 18, 2013

ZAIDI ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule mbali mbali za Sekondari Wilayani Chunya Mkoani Mbeya wameshindwa kuripoti Mashuleni


Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, amewataka Wazazi wa Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao Shuleni haraka kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi agizo hilo.




ZAIDI ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule mbali mbali za Sekondari Wilayani Chunya Mkoani Mbeya wameshindwa kuripoti Mashuleni kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kujiingiza katika biashara za uchimbaji wa Madini na Uvuvi.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, amewataka Wazazi wa Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao Shuleni haraka kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi agizo hilo.
Kinawiro aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Majengo kata ya Sangambi Wilayani humo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Afisa elimu wa Wilaya kuhusu kukithiri kwa utoro wa wanafunzi mashuleni, Hivyo kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo yake ya kufuta ujinga miongoni mwa wananchi.
Alisema Wilaya ya Chunya inakabiliwa na Wimbi kubwa la wafugaji wenye tabia ya kuhamahama jambo ambalo husababisha kuwakatisha masomo wanafunzi ili hali wengine wakijikita kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi katika Ziwa Rukwa.
Alisema kufikia Mwishoni mwa mwezi huu mzazi yeyote ambaye hatampeleka Mwanaye Shule bila kujali kisingizio cha aina yoyote atakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumwachisha masomo mwanafunzi na kumpatia ajira kinyume cha Sheria.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema Idadi ya watoto 500 ni kubwa sana hivyo hali hiyo ikiachwa itazalisha Wajinga wengi jambo ambalo litakuwa mzigo kwa taifa kutokana na wengine kuwa majambazi baada ya kukosa fedha kutokana na ajira walizojiingiza katika umri mdogo na kukwamisha juhudi za Serikali za kujenga Shule katika kila kata.
Kinawiro alisema Wilaya ya Chunya kitaaluma inafanya Vizuri katika ngazi ya Mkoa ukilinganisha na Wilaya zingine hivyo hayuko tayari kuona sifa hiyo inapotea kutokana na wazazi wachache kuzembea na kutokujua umuhimu wa kumsomesha mtoto, na kuongeza kuwa Halmashauri inaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuimarisha ujenzi wa Mabweni ili kuhakikisha watoto wa kike hawakatizwi masomo kutokana na mimba zisizotarajiwa.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wafugaji wote waliohamia Wilayani Chunya kinyume cha Sheria kuondoka mara moja na atakae kaidi agizo hilo atakumbana na Operesheni kubwa ya kuwaondoa kwa nguvu ambapo kwa sasa wanafanya doria kwa kutumia ndege maalumu ili kuwabaini wahamiaji hao.
Alisema zoezi hilo litafanyika hivi karibuni baada ya kumalizi kuwabaini wafugaji waliovamia misitu na sehemu za hifadhi ambapo wanaharibu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo huharibu mazingira ya Chunya kwa Ujumla.
  
Hivi karibuni kulifanyika zoezi la kuwaondoa wafugaji waliovamia msitu wa hifadhi wa kijiji cha Mbangala ambapo Jumla ya mifugo 1000 ilikutwa msituni humo na kufanyika uharibifu mkubwa lakini zoezi hilo liliingiliwa na hitilafu baada ya wafugaji hao jamii ya Wamang’ati kuwashambulia kwa mishale na mikuki maofisa pamoja na Askari wa Jeshi la Polisi waliokimbia kunusuru maisha yao.
Na E . Kamanga Chunya 

No comments:

Post a Comment