Pages

Tuesday, May 7, 2013

SIRI NZITO YAFICHUKA NA YA YULE MFANYA BIASHARA ALIYE JIRUSHA GHOROFANI KARIAKOO!

NYUMA ya habari ya mfanyabiashara tajiri wa Kariakoo jijini, Costa Shirima (47), anayedaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, Dar es Salaam na kufariki dunia, kuna siri ambayo Ijumaa Wikienda limeelezwa.

Wananchi wakiwa eneo alipodondoka marehemu Costa Shirima.


Habari za kina kutoka hotelini hapo zilieleza kuwa Shirima alikuwa asafiri kwa ndege ya saa 10:00 jioni, Ijumaa iliyopita kuelekea nchini China kufuata bidhaa za maduka yake.


ALIMILIKI MADUKA KADHAA

Uchunguzi wa Ijumaa Wikienda ulibaini kwamba Shirima ambaye alithibitishwa kufariki dunia baada ya kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar, alikuwa akimiliki maduka kadhaa ya urembo wa akina mama yaliyopo jirani na hoteli hiyo ya Concord.

Taarifa zaidi zilidai kuwa marehemu mara kwa mara alikuwa akipendelea kula katika hoteli hiyo na siku ya tukio inadaiwa kuwa aliwaeleza watu kuwa anapanda juu ya hoteli hiyo kupunga upepo.

Ilidaiwa kuwa jamaa zake walipomhoji kulikoni kwenda kupunga upepo mchana wote huo, Shirima alisema kuwa alihisi hewa nzito mahali alipokuwa.


Mwili wa Costa Shirima baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, jijini Dar.


MHUDUMU AFICHUA MANENO YA MWISHO

Madai zaidi yalishushwa na mhudumu mmoja wa hoteli hiyo aliyeomba hifadhi ya jina kuwa jamaa huyo alipoingia mahali hapo, alitaka kupatiwa chumba cha kupumzika lakini alipopelekwa kwenye vyumba vya ghorofa ya kwanza alikataa hadi alipofika ya tisa na kuanza kupunga upepo.


Mhudumu huyo alidai kuwa alikuwa akimsikia Shirima akiongea peke yake akisema “Haiwezekani… haiwezekani kabisa…” na baadaye alipokea simu ya kiganjani ambayo alisikika akibishana na mtu wa upande wa pili.

Kwa kuwa kila mtu alikuwa na shughuli zake, inadaiwa kuwa ghafla watu walishtushwa na kishindo na kumuona akiwa chini, akiwa amedondokea gari dogo aina ya Toyota Corola linalofanya biashara ya teksi ambalo liliharibika vibaya kutokana na kuangukiwa.

Marehemu Shirima mbali ya kuwa mfanyabiashara wa muda mrefu Kariakoo, pia alikuwa akiendelea na ujenzi wa jengo lake la ghorofa maeneo hayo.

Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, Dar es Salaam alipokuwa Shirima.


SIRI NYINGINE

Kuna madai kwamba siku moja nyuma alikuwa akilalamikia taratibu za mikopo katika mabenki na kwamba kuna watu wa benki walimfuata akawa anajibishana nao.

Madai mengine ni kwamba inawezekana kuna mtu alikuwa akimtuma kwenda kulipia bili, kodi ya mapato na vitu mbalimbali, hivyo kuna uwezekano alikuwa hapeleki sehemu husika hivyo kumweka katika wakati mgumu.


...Shirima baada ya kujirusha kutoka ghorofani.


TARATIBU ZA MAZISHI

Shirima ameacha mjane na watoto watano, alikuwa akiishi Kimara Suka ambapo taratibu za mazishi zinafanyika na mwili unatarajiwa kusafirishwa kwenda Mwika, Moshi kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika kesho Mei saba mwaka huu.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marieth Minangi, uchunguzi wa tukio bado unaendelea na taarifa kamili zitatolewa ukikamilika. “Tukio kweli limetokea na uchunguzi bado unafanyika,” alisema Kamanda Minangi.

No comments:

Post a Comment