Pages

Saturday, May 18, 2013

WANAFUNZI 15 WAKAMATWA NA POLISI MBEYA


RPC  Mbeya Diwani Athuman
Na Esther Macha, Mbeya
WANAFUNZI kumi na tano(15) katika shule ya sekondari ya Wazazi ya Lupata Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kuchoma moto bweni la shule hiyo kutokana na wanafunzi wenzao kusimamishwa masomo  na uongozi wa shule kwa utovu wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ,Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya Bw.Diwani Athuman alisema kuwa tukio lilitokea mei 14 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika shule ya sekondari Lupata.
Bw.Athuma alisema kuwa wanafunzi hao baada ya kuona wanafunzi wenzao watatu wamesimamishwa  masomo walianza  vurugu usiku na kuanza kuchoma moto  bweni moja  la wanafunzi wa kiume .
Aidha Kamanda Athuma aliwataja wanafunzi waliosimamishwa kwa utovu wa  nidhamu shuleni hapo kuwa  ni ,Joseph Robert (18) Kidato cha nne Mkazi wa Kitunda Jijini Dar es Salaam,Mwita Chacha(17),Mwanafunzi wa  kidato cha tatu  mkazi wa Jijini Dar es Salaam ,pamoja  na Daniel David(18)kidato cha Tatu mkazi wa Ipinda Kyela.
 “Hawa wanafunzi watatu waliosimamishwa masomo walihamasisha wenzao kuunga mkono kupinga adhabu hiyo  kwa kufanya  vurugu na kuchoma bweni hilo la wanafunzi”alisema Kamanda Athuman.
Alisema kuwa  bweni lilochomwa moto walikuwa wanaishi wanafunzi ambao hawakuwa tayari  kuunga mkono uvunjifu huo wa amani shuleni hapo.
Aidha Bw. Athuman alisema kuwa kufuatia  vurugu hizo vinara wawili wa vurugu hizio wanashikiliwa na jeshi kwa mahojiano zaidi ambao ni ,Joseph Robert , Mwita Chacha huku  watuhumiwa kumi na tano wanashikiliwa na jeshi hilo.
Kuhusu vitu ambavyo vimeharibiwa Kamanda huyo alisema thamani halisi ya uharibifu uliotokea bado kujulikana na kwamba hakuna madhara yeyote ya kibinadamu  yaliyotokea .
Hata hivyo Bw.Athuman ametoa wito kwa jamii  hasa wanafunzi kuacha tabia  ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake watatue matatizo  kwa njia ya meza ya mazungumzo katika mamlaka husika ili kuepusha madhara na hasara zinazoweza kujitokeza ambazo mara nyingi wahanga wanakuwa ni wanafunzi wenyewe.

No comments:

Post a Comment