Pages

Thursday, May 9, 2013

Chanjo ya Ukimwi yaonyesha mafanikio

 

 

 

 

 

 

Dk Hussein Mwinyi 

 

Matokeo ya awali ya chanjo ya dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi yaliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) yameonyesha kuwa chanjo hiyo ni salama na ina uwezo wa kusisimua mwili na kuzalisha viini kinga katika dozi ndogo.

Akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Mwaka wa Fedha wa 20013/2014, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema chanjo hiyo aina ya TAMOVAC-01 imeshirikisha watu 60 katika Mkoa wa Mbeya.

Hii ni mara ya pili kwa Serikali kufanya utafiti kama huo. Mara ya kwanza ulihusisha wanajeshi, askari polisi na magereza wapatao 60 wa Dar es Salaam ambao walipewa dawa na kuachwa waendelee na maisha yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.

Hata hivyo, alipoulizwa jana jioni kuhusu utafiti huo wa awali ulipoishia Dk Mwinyi alisema: “Huu ni utafiti mwingine ule wa awali ulikatizwa.” Alisema utafiti wa awamu ya pili unaendelea na umeonyesha mafanikio makubwa.

 

Alisema taasisi hiyo pia iliendelea na utafiti wa awamu ya tatu wa chanjo ya malaria iitwayo RTS, S/AS01E na matokeo yake kwa watoto wa rika la wiki sita hadi 12 yalionyesha kuwa ina ubora sawa na chanjo zitolewazo kwa watoto na inazalisha viini kinga.

“Chanjo hii ilipunguza watoto kuugua malaria mara kwa mara kwa kiwango cha asilimia 30 kwa mwaka mmoja wa ufuatiliaji,” alisema.

Alisema utafiti huo ulihusisha vijiji 34 vya Wilaya za Handeni na Korogwe na jumla ya watoto 1,505 chini ya miezi 17 walipata chanjo ya malaria au chanjo ya kilinganishi na walikamilisha kupatiwa dozi ya nyongeza ilipofikia robo ya nne ya mwaka 2012 na ufuatiliaji unaendelea.

Alisema Serikali imepata mafanikio katika juhudi za kudhibiti magonjwa ya Ukimwi na malaria kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2011/12 kuhusu viashiria vya magonjwa hayo kuonyesha kuwa malaria imepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007/08 hadi asilimia 10 mwaka 2011/12.

Alisema taasisi hiyo itaendelea na utafiti wa chanjo dhidi ya Ukimwi na awamu hii itahusisha washiriki 80 katika Mkoa wa Mbeya lakini pia itaendelea na hatua ya kwanza ya utafiti ujulikanao kama R 262 utakaochunguza aina nyingine ya chanjo ya DA na MVA dhidi ya Ukimwi kwa lengo la kubaini ubora na usalama wa chanjo hiyo mpya kwa kuchanja washiriki 20 mkoani Mbeya.

Waziri Mwinyi alisema wizara imeomba cha Sh47,282,941,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambao kati ya fedha hizo Sh36,1000,000 ni fedha za ndani na Sh435,182,941,000 zinatoka kwa asasi za kimataifa na wadau wa maendeleo.

 

Alipoulizwa baadaye sababu za bajeti hiyo kuwa tegemezi kwa zaidi ya asilimia 80, alisema Serikali imeamua kupeleka fedha nyingine katika matumizi mengine ya msingi baada ya kuhakikishiwa kupatiwa fedha na wahisani.

Alisema wizara pia imepanga kuajiri wataalamu 612 wa kada mbalimbali na kuwapandisha vyeo watumishi 707.

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Antony Mbassa alizungumzia tatizo la dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV) na kuitaka Serikali kutoa taarifa juu ya makopo 4,000 kama yameondolewa sokoni ili watumiaji wasiathirike.

Mwaka jana gazeti la Mwananchi lilifichua taarifa za kuwapo ARV bandia sokoni baadhi zikiwa zimeanza kutumiwa.

 

No comments:

Post a Comment