Pages

Tuesday, May 7, 2013

Dk Nchimbi Wasio Ipenda Nchi yetu Wanapandikiza Chuki za Udini





“Tutachukua hatua kali bila huruma kuzigandamiza njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu. Tutachukua hatua kali kwa mtu yeyote bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii. Amani yetu kwanza na taifa letu kwanza,” alisema Waziri Nchimbi

NA IMMACULATE MAKILIKA- MAELEZO

SERIKALI imesema kuwa itachukua hatua kali kwa mtu yeyote bila kujali hadhi nafasi yake katika jamii kufuatia kuwepo kwa watu wachache wasiyoitakia mema nchi yetu kutaka kupandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta mapigano, mauaji nchini

Kauli hiyo imetolewa Bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu mlipuko uliotokea katika kanisa la katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti Arusha mjini Mei 5, mwaka huu saa 4:30 asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi 59, kati ya hao watatu ni mahututi.

Aliwataja watu waliofariki dunia kuwa ni Regina Kurusei mwenye wa miaka 45 mkazi wa Olasiti ambaye alifariki siku ya tukio wakati alipokuwa kipatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru na James Gabriel(16) aliyefariki usiku wa kuamkia 06/05/2013.

“Tutachukua hatua kali bila huruma kuzigandamiza njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu. Tutachukua hatua kali kwa mtu yeyote bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii. Amani yetu kwanza na taifa letu kwanza,” alisema Waziri Nchimbi.

Alisema tayari kikosi kazi maalumu kimeundwa ili kuchunguza tukio hilo.
Waziri Nchimbi alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko huo ni bomu. Hivyo uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na Wataalamu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania .

“ Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na jeshi la polisi. Miongoni mwao ni Victor Ambroce mwenye umri wa miaka 20, dereva wa bodaboda,mkazi wa Mrombo, Arusha,ambaye anatuhumiwa kwa kurusha bomu hilo. Watuhumiwa wengine watano waliokamatwa ni raia wane wa kigeni na Mtanzania mmoja ambao wanashikiliwa kwa maahojiano,” alisema.

Aidha Waziri Nchimbi alisema Serikali inamewataka wanasiasa na viongozi wote wajiepushe na kauli zinazochochea ubaguzi wa kidini, mifarakano ya kijamii na chuki miongoni mwa Watanzania.
”Serikali isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria itakazozichukua dhidi ya viongozi wa aina hii ambao maslahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania, maslahi yao ni muhimu kuliko umoja wa Watanzania,” alisisitiza huku akisema Serikali kwa nguvu zake zote itahakikisha kuwa watuhumiwa wote waliohusika na kushiriki kwa namna yoyote katika tukio hilo wanasakwa popote walipo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aliongeza kuwa kwa niaba ya Serikali anaungana na Watanzania kulaani wahusika wote wa tukio hilo walioshiriki kwa njia yoyote. Pia inawataka viongozi wa kisiasa, kidini,na wananchi wote kwa ujumla kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu.


Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada ya uzinduzi wa Parokia, mgeni rasmi alikuwa Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Fransisco Mantecillo Padilla. Aidha alikuwepo mwenyeji wake Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha.

Inakadriw a kuwa katika uzinduzi huo kulikuwa na watu zaidi 2000. Hivyo wakati mgeni rasmi akiwa ametoka nje akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi mtu aalirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi kuelekea eneo kulipokuwa na mkusanyiko wa watu na baada ya kutua kulitokea kishindo na mlipuko mkubwa.
Katika tukio hilo viongozi wa Serikali na dini waliohudhuria ibada hiyo hawakupata madhara.

No comments:

Post a Comment