Pages

Thursday, May 9, 2013

• Dk. Slaa: CHADEMA hatutalipa kisasi

Slaa afunguka

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema hawatalipa kisasi hata baada ya mahakama kumfutia kesi ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho, Wilfred Lwakatare, kwa kigezo kuwa mashitaka hayo yalikuwa hayajitoshelezi kuitwa kuwa ni ya ugaidi.

Akizungumza na gazeti hili baada ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kuvutia hisia za watu wengi Dk. Slaa alisema:

“Tumesema toka mwanzo, tunaanza na Mungu, tunaendelea na Mungu na tutamaliza na Mungu, hujuma zozote dhidi ya CHADEMA kamwe hazitashinda kwa uwezo wa Mungu. CHADEMA tunapigania ukombozi wa pili wa taifa letu, tunawapigania wanyonge, tunawapigania walalahoi. Hatukuwa, hatuna na hatutakuwa na sababu ya ugaidi.

“Tunachopigania ni haki za msingi za Watanzania wa makundi yote, tunawashukuru wananchi wote waliotuombea, waliotufariji na kututakia mema kipindi chote tulipobambikizwa kesi ya ugaidi, tukatukanwa matusi ya kila aina. Hatutalipa kisasi kwa waliotubambikizia kesi na tunawajua wote, haki itatendeka.”

 

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana ilimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.

 

Jaji Lawrance Kaduri alitoa uamuzi huo jana na kusema ulitokana na ombi la mawakili wa Lwakatare; Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabere Marando la kutaka mahakama hiyo ipitie mwenendo mzima wa majalada ya kesi Na. 37 na 6 za mwaka huu zilizopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, alitumia madaraka yake kinyume cha sheria kuifuta kesi namba 37 ya mwaka huu.

Makosa yaliyofutwa ni la kula njama lililokuwa likiwakabili washitakiwa wote ambalo ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002, ambapo walidaiwa kutaka kumteka Denis Msaki kinyume cha kifungu cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Shitaka la tatu ni la kupanga kufanya makosa ya ugaidi kinyume cha kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msaki kinyume cha kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Shitaka la nne, ambalo linamkabili Lwakatare pekee, ni la kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume cha kifungu cha 23(a) cha Sheria ya kuzuia ugaidi, kwamba Desemba 28 mwaka jana, akiwa ni mmiliki wa nyumba iliyopo Kimara King’ong’o kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki.

Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Kaduri alisema amekubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare ya kuwa shitaka la pili, tatu na la nne hayaoneshi kama Lwakatare alikuwa na nia ya kutenda kosa la ugaidi, hivyo Lwakatare atabakia na shitaka la kwanza ambalo ni kula njama kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki ambaye ni Mhariri wa Habari wa gazeti la Mwananchi.

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama inatoa amri ya kumfutia Lwakatare mashitaka matatu, yaani kosa la pili, tatu na la nne kwa sababu Jamhuri imeshindwa kuonesha maelezo yanayotesheleza kumshitaki Lwakatare kwa kesi ya ugaidi.

“Naamuru jalada la kesi ya msingi lilirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya mshitakiwa kuendelea kushitakiwa kwa kosa moja la kula njama ambalo linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002,” alisema Jaji Kaduri.

Hata hivyo, Jaji Kaduri alitupilia mbali hoja ya mawakili wa Lwakatare iliyodai DPP alitumia madaraka yake vibaya ya kufuta kesi na kuifungua upya, ambapo alisema anakubaliana na hoja ya mawakili wa serikali, Prudence Rweyongeza na Ponsian Lukosi kuwa uamuzi wa DPP ulikuwa sahihi kisheria.

 

No comments:

Post a Comment