Pages

Tuesday, May 7, 2013

Mkosamali ni mbunge halali - Mahakama


MAHAKAMA ya Rufaa nchini imetupilia mbali rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Muhambwe, wilayani Kibondo, iliyofunguliwa na Jamal Abdalah Tamimu (CCM) dhidi ya Felix Mkosamali (NCCR – Mageuzi).

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji, Nathalia Kimaro na William Mandia, waliokuwa wakisikiliza shauri hilo Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Themistocles Kaijage, alisema Mahakama ya Rufaa imeamua kufuta shauri hilo baada ya mrufani kutotimiza masharti ya kisheria.

Jaji Kaijage alisema kwamba Mahakama ya Rufaa imekubaliana na hoja za mlalamikiwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Muhambwe (NCCR-Mageuzi ) kuwa mrufani Jamal Tamim, hakutimiza masharti ya kisheria ikiwemo kukosekana kwa kumbukumbu muhimu katika hati asilia ya malalamiko.

Wakili wa mjibu rufaa, Raymond Kabuguzi, alidai mbele ya jopo hilo kuwa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu iliyosikiliza shauri hilo hapo awali pia hayakuambatanishwa.

Kufuatia kutupwa kwa rufaa hiyo namba 110/2012, Mbunge wa jimbo la Muhambwe, lililoko, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, anabaki kuwa Felix Francis Mkosamali.

Wakili wa mbunge huyo Raymond Kabuguzi, aliweka pingamizi kuwa rufaa iliyofunguliwa haikukamilika kwani ilikuwa inakosa kumbukumbu muhimu zilizopaswa kuambatanishwa na rufaa husika hivyo isikubaliwe kupokelewa na kusikilizwa.

Mwanasheria mkuu wa serikali aliwasilishwa na wakili mkuu wa serikali, Obadia Kameya, pia alikiri kukiukwa kwa taratibu za kisheria hivyo kuungana na hoja za wakili mjibu rufani wa kwanza.

Kufuatia hoja hizo za mjibu rufani wa kwanza na mjibu rufani wa pili, mwanasheria mkuu wa serikali, Mahakama ya Rufaa imeamua kufuta shauri hilo na kumthibitisha Felix Mkosamali kuwa mbunge halali wa jimbo la Muhambwe.

Katika shauri la msingi mahakama kuu, mrufani Jamal Tamim, alidai kuwa Mkosamali hakushinda kihalali kwani taratibu zilikiukwa na kutaka ubunge wake utenguliwe na mahakama kuu.


No comments:

Post a Comment