Pages

Tuesday, May 7, 2013

Serikali yaahidi kujenga minara ya simu Ludewa

Kwa ufupi

“Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) inaendelea na jitihada zake kuhakikisha maeneo yote nchini hususan vijijini yanapata huduma za mawasiliano ya simu,” alisema Kitwanga.

Dodoma.

Serikali imesema itaanza ujenzi wa minara maeneo ya Jimbo la Ludewa yasiyofikiwa na huduma za mawasiliano ya simu kwa mwaka fedha 2013/14.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM).
Katika swali lake, Filikunjombe alitaka kujua mpango wa Serikali kujenga minara ya simu eneo la mwambao wa Ziwa Nyasa na Milimani. Filikunjombe alisema wananchi wanalazimika kupanda juu ya miti kupata mawasiliano.
Kitwanga alisema ujenzi wa minara hiyo utagharimiwa kupitia fedha za Benki ya Dunia (WB), zabuni ya kwanza itatangazwa Mei mwaka huu.
Alivitaja vijiji ambavyo havina mawasiliano kuwa ni Chanjale, Lumbila, Nkanda, vijiji vya Kata ya Madilu, Lupingu, Mtumbati, Nindi, vijiji vya Kata za Kilondo, Makonde na Madope.
“Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) inaendelea na jitihada zake kuhakikisha maeneo yote nchini hususan vijijini yanapata huduma za mawasiliano ya simu,” alisema Kitwanga.
Naibu waziri huyo alisema lengo ni kuhakikisha maeneo yasiyofikiwa na watoa huduma yanafikiwa kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwamo ruzuku inayotolewa na UCAF kushawishi kampuni za simu kupeleka mawasiliano maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment