Pages

Wednesday, May 8, 2013

Dk. Nchimbi amtega Tundu Lissu


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, amemtaka Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kugombea urais ili aweze  kufukuza  kazi mawaziri.

 Akichangia hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014, Lissu alitaka Dk. Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema, wajiuzulu ama wafukuzwe kazi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hali iliyosababisha chokochoko zinazoendelea. 

Dk. Nchimbi aliyasema hayo jana bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/2014.

Alisema watu wanahangaika barabarani kuomba kura maana yake wanatafuta mamlaka ya kufukuza na kuajiri watu.

Alisema kuwa wengine wamekuwa wakianzisha ofisi zao ili wapate mamlaka hiyo ya kufukuza na kuajiri watu. 

“Mtu atanishangaa sana akiniona nimekwenda Chadema na kusema Katibu Mkuu  huyu hafai fukuza, ulimweka wewe?” alihoji na kuongeza:

“Moja ya  ya mbinu rahisi sana za kujua kuwa Nchimbi kachanganyikiwa ni kwenda Chadema na kutamka amfukuze Katibu Mkuu wenu. Kama una hamu ya kufukuza mawaziri gombea urais.”

 Kuhusu suala la udini, Dk. Nchimbi alisema unapoomba kura kupitia makanisani kwa mapadri na wachungaji, watu wakisema wewe ni mdini hautakiwi kulalamika.

“Ukiomba kura kupitia misikitini, kupitia masheikhe na maimamu watu wakisema wewe ni mdini usilalamike unatakiwa kuacha,” alisema. 

Aliwataka watu waliotumia njia hiyo kupata kura, kujirekebisha wenyewe iwapo wanafahamu waliomba kura kupitia katika makanisa na misikiti  maana kujirekebisha ni uungwana. 

Kwa upande wa malalamiko ya kambi ya upinzani kuwa wamekuwa wakizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, Dk. Nchimbi alikipongeza Chadema kwa kauli yao kuwa ndicho kilichofanya mikutano mingi kuliko vyama vyote.

 Alisema kuwa  pongezi hizo ziambatane na pongezi za polisi kuwa walifanya kazi nzuri katika kusimamia mikutano hiyo ya Chadema.

 Alisema maelekezo ya Jeshi la Polisi kutofanya kwa kuzingatia maelekezo ya wanasiasa wanayafanya na wataendelea kufanya hivyo.

 Akizungumza kuhusiana na kulivunja Jeshi la Polisi na kuliweka kama kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Dk. Nchimbi, alisema hayo ni makosa madogo madogo yaliyopo katika jeshi hilo na si ya kusababisha kulivunja. 

Kuhusu suala la matumizi mabaya ya simu, Dk. Nchimbi, alisema  kuwa kumekuwa na matatizo katika mitandao ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu kutotumika kikamilifu.



No comments:

Post a Comment