Pages

Wednesday, May 8, 2013

Waziri Kawambwa apigwa kombora


Wadau wa elimu nchini wamezidi kumbana na kumshinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ajiuzulu kwa hiari ama serikali imuondoe kwa nguvu kwa madai kuwa amesababisha hasara na aibu kwa taifa kufuatia kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 yasiyo sahihi.

Kadhalika, wadau hao wamesema kitendo cha serikali kufuta matokeo hayo ili kuyapanga upya kimeharibu taswira ya nchi kimataifa katika sekta ya elimu.

Msimamo huo ulitolewa kwa pamoja jana jijini Dar es Salaam kwa waandishi wahabari na mashirika matano yasiyokuwa ya serikali ya Sikika, TGNP, HakiElimu, Policy Forum na  Ten/Met.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, Elizabeth Missokia, akizungumza na waandishi wa habari, alisema wadau hao wamekutana ili kuweka msimamo juu ya kauli iliyotolewa na serikali ya kufuta matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012.

Missokia alisema serikali ilitakiwa kupima na kufanyia majaribio mfumo wa kuweka madaraja ya ufaulu katika mitihani hiyo kabla ya kutangaza matokeo ili kuona kama unafanya kazi vizuri.

Aliongeza kuwa wadau wa elimu nchini hawajui faida zilizopo katika mfumo mpya uliotumiwa na serikali kupanga matokeo hayo ambayo alidai yamelitia aibu taifa.

Hata hivyo, Missokia aliitaka serikali itakapofanya zoezi la kupanga madaraja upya baada ya kufuta matokeo liwe la wazi na wadau wote washirikishwe badala ya kazi hiyo kufanyika kwa usiri.

“Hili zoezi lifanyike kwa uwazi na kila mdau apate fursa ya kushiriki ili kujua kitakachokuwa kinaendelea kwa kuwa matokeo mabaya yameendelea kutokea tangu mwaka 2006 hadi sasa na hili ni jambo la hatari,” alisema Missokia.

Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Ushauri wa HakiElimu, Nyanda Shuli, alimtaka Dk. Kawambwa kupima mwenyewe juu ya kujiuzulu kwa kuwa mambo mengi yamekuwa yakijitokeza katika uongozi wake.

Alisema ni wakati mwafaka kwa serikali kumuwajibisha, Dk. Kawambwa kutokana na makosa anayoyafanya katika kusimamia sekta ya elimu nchini pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara yake.

Naye Mratibu wa Ten/ Met, Cathleen Sekwao, alisema alishangaa kusikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anaunda tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 wakati sababu zake zinajulikana wazi.

Wadau hao walisema madhara katika sekta ya elimu nchini yataendelea kuwapo kwa kuwa kuna wasiwasi baadhi ya wanafunzi watakaoendelea na masomo ya kidato cha tano hawatakuwa na sifa kutokana na serikali kuvurunda katika kupanga matokeo ya mwaka  2012.

Wiki iliyopita serikali ilichukua uamuzi mgumu na kufuta matokeo kidato cha nne ya mwaka 2012.

Uamuzi huo mgumu ulifanywa na Baraza la Mawaziri kabla ya tume ya Waziri Mkuu kuwasilisha ripoti yake kama njia ya kuwafariji wanafunzi waliofeli mtihani na kulitaka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kuyapanga upya kwa kutumia utaratibu wa kupanga madaraja uliotumika mwaka 2011.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akiwasilisha kauli ya serikali bungeni mjini Dodoma Ijumaa iliyopita, alisema utaratibu mpya uliotumika kupanga madaraja ulichangia katika matokeo mabaya yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri.

Februari mwaka huu, Dk. Kawambwa alitangaza matokeo ya kidato cha nne na kubainisha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 walipata daraja la nne.

Watahiniwa walikuwa 456,137 kati yao wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea 68,806.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.

Matokeo hayo yaliibua mjadala mkali huku makundi mbalimbali ya jamii yakihoji sababu zilizosababisha wanafunzi wengi kufeli na kutaka Kawambwa na wasaidizi wake wawajibike kabla Waziri Mkuu kuunda tume iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza ili kupata ufumbuzi wa kudumu.


No comments:

Post a Comment