Pages

Sunday, May 12, 2013

Polisi: Bomu Arusha siyo la kienyeji


 

Kamanda wa Polisi Arusha, Lebaratus Sabas  

 Siku saba baada ya tukio la mlipuko wa bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,Olasiti mkoani Arusha, Jeshi la Polisi limesema kuwa mlipuko huo ulitokana na bomu lililotengenezwa kiwandani.
Taarifa hiyo ni sehemu ya matokeo ya uchunguzi unaofanywa kutokana na tukio hilo lililotokea Jumapili iliyopita, kupoteza maisha ya watu watatu na kujeruhi wengine 67 baadhi wakiwa katika hali mbaya.
Polisi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) vipo katika uchunguzi kuhusu tukio hilo lililotokea muda mfupi kabla ya kanisa hilo kuzinduliwa rasmi ambapo mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Francisco Padilla.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa bomu hilo siyo la kutengenezwa kienyeji, bali ni la kiwandani.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha, bomu lililotupwa kanisani siyo la kutengeneza kienyeji. Hii ni kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka kwa wataalamu ndani ya Jeshi la Polisi,” alisema na kuongeza:
“Taarifa kamili itatolewa Jumatatu (kesho) kwa kuwa kuna baadhi ya watuhumiwa wanaendelea kukamatwa na kuhojiwa na polisi na wengine watafikishwa mahakamani.”
Kamanda Sabas alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na halitasita kutoa taarifa kwa umma kukiwa na haja ya kufanya hivyo, ambapo amewaomba wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia upelelezi kuzitoa polisi.
Arusha na Ugaidi
Taarifa hizo zimekuja huku mji wa Arusha ukianza kuingia katika rekodi mbaya ya kuhusishwa na vitendo vya ugaidi, baada ya matukio matatu kuuhusisha mji huo wa kitalii nchini.
Kuhusishwa kwa mji huo na ugaidi kunatokana na wahusika wakuu wa milipuko iliyotokea nchini na nchi jirani kudaiwa kwamba waliratibu vitendo hivyo wakiwa katika mji huo.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 1998 mtuhumiwa mkubwa wa ugaidi, Ahmed Khalfan Ghailani, alidaiwa kukaa kwa muda mjini Arusha na kununua baruti za kulipulia miamba kutoka kwa baadhi ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mirerani, Wilaya ya Simanjiro.
Baadaye ilibainika kuwa mabomu yaliyotumika kulipua Ofisi za Ubalozi wa Marekani katika miji ya Dar es Salaam na Nairobi nchini Kenya katika tukio la Agosti 7, mwaka huo wa 1998, malighafi zake zilinunuliwa mkoani Arusha na Ghailani.
Katika tukio jingine la mwaka 2011, wakazi wawili wa Arusha, Abdulmalik Majid na Hija Seleman Nyandondo (30), walikamatwa kwa tuhuma za kushiriki njama za kuilipua kwa bomu klabu moja ya usiku katika Jiji la Kampala nchini Uganda lililopoteza maisha ya watu 74, waliokuwa wakitazama mpira wa Fainali za Kombe la Dunia, mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment