Pages

Wednesday, May 15, 2013

Aliyejeruhiwa kwa bomu apoteza jicho


Mfanyabiashara Apolnary Malamsha (33)  wa Arusha ambaye jicho lake limepata hitilafu baada ya kutobolewa na chuma cha bomu wiki mbili zilizopita akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jana.

 

 Mfanyabiashara Apolnary Malamsha (33) amejikuta katika wakati mgumu baada ya kuelezwa kuwa chuma cha bomu kilichomtoboa chini ya jicho la kushoto kimeingia ndani na kumharibia mfumo wa kuona.

Akizungumza kwa masikitiko juzi katika wodi namba ya 10  Kibasila kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alipolazwa, Malamsha ambaye ni mkazi wa Olasiti Arusha alisema taarifa hiyo imemsikitisa na kumuogopesha.

“Nimechunguzwa na daktari ameniambia kwamba kipande cha chuma kilichotoboa jicho langu kiliingia ndani na kukata mojawapo ya mishipa inayowezesha jicho kuona kwa hiyo hakuna uwezekano wa kuona tena,” alisema kwa masikitiko Malamsha.

Malamsha pia anasumbuliwa na kutapika, hali ambayo anadai inachangiwa na vyuma vya mabomu vilivyoingia mwilini mwake.

Naye kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Priscus Malamsha ambaye alikuwa akimhudumia alieleza kuhuzunishwa na habari hizo kwa kuwa inaweza kumpunguzia mdogo wake furaha ya maisha yake.

“Najisikia vibaya huyu ni mdogo wangu, lakini bomu limemfanya apoteze furaha yake, tazama anavyotapika kila anachokula, lakini tutaendelea kumtazama Mungu,” alisema Malamsha ambaye naye ni mkazi wa Olasiti.

Kijana huyo ni miongoni mwa majeruhi  saba waliofikishwa MNH kwa matibabu zaidi, baada ya kujeruhiwa kwenye mlipuko wa bomu uliotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakafitu Joseph Mfanyakazi.

Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa MNH, Jeza Waziri alieleza kuwa majeruhi karibu wote wanaendelea vyema,baadhi yao wanaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani kwao hasa kutokana na hali zao kuendelea kuimarika.

Majeruhi wengine ni Gabriel Godfery (9),  Jenipher Joachim (40) na Anastazia Regnard (14).

Wengine ni Albert Njau (35),  Faustine Shirima (33) Fatuma Tarimo (38)  ambaye  amepimwa na kuonekana ana  chembechembe za vyuma vya bomu ndani ya tumbo lake.



No comments:

Post a Comment