MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA),
amehoji ni lini serikali itarekebisha mwonekano ulioanza kujitokeza kwa
Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kutoa habari kwa kukipendelea
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kwa kuwa wakati wa uongozi wa Tido Mhando TBC ilionekana kama ndege
ambayo inapaa na kuwafanya Watanzania wengi kujenga imani na chombo
hicho kwa maana ya kupata habari za uhakika na zisizo na upendeleo…
“Lakini kwa sasa shirika limekuwa kama ndege ambayo inarudi chini
kutokana na kushindwa kutoa habari kama ilivyokuwa awali na sasa imekuwa
ikitangaza habari za upendeleo wa kukibeba chama tawala (CCM). Je,
serikali ina kauli gani kwa wananchi kuwa sasa wataanza kujenga imani na
chombo hicho ambacho kimeishaanza kupoteza imani kwa wananchi?” alihoji
mchungaji Msigwa.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Abdulla Amour
(CUF) alitaka kujua ni mikoa mingapi inakosa matangazo ya TBC hadi sasa.
Aidha, alitaka kuelewa serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha shirika hilo linasikika kwa kurusha matangazo yake nchi nzima.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Amoss Makala, alisema si kweli shirika hilo linatangaza habari
zake kwa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Makala alisema mikoa ambayo haipati matangazo ya redio ni tisa ambayo
ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Kaskazini Pemba,
Kusini Pemba, Geita, Mtwara, Njombe na Simiyu.
|
|
No comments:
Post a Comment