Rais Jakaya Kikwete
Kuna kila dalili kwamba wabunge
wa CCM wameanza kupanga majeshi kwa lengo la ‘kumalizana’ watakapokutana
kwa siku mbili mfululizo na mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais
Jakaya Kikwete.
Mkutano huo unaotajwa kuwa zao la jitihada za
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana unatarajiwa kufanyika kesho na
keshokutwa mjini Dodoma, huku kukiwapo taarifa kwamba wabunge
wamegawanyika katika makundi kwa lengo la kupenyeza, kisha kutetea hoja
walizonazo dhidi ya wenzao.
Miongoni mwa hoja zinazotajwa ni ile ya
kushughulikiwa kwa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa kwamba ni wapinzani
ndani ya CCM, wakiwamo, Alphaxard Kangi Lugora (Mwibara), Deo
Filikunjombe (Ludewa), Ally Keissy Mohamed (Nkasi Kaskazini) na Luhaga
Mpina (Kisesa).
Wabunge hao wanatuhumiwa na wenzao kwamba
wanawasaidia wapinzani kutokana na misimamo yao ya kuikosoa hadharani
Serikali katika vikao na mikutano tofauti ya Bunge.
Itakumbukwa kuwa Aprili 25 mwaka huu baada ya
kukwama kwa Bajeti ya Wizara ya Maji, wabunge wa CCM walikutana katika
kikao cha dharura kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambako
Lugola na Filikunjombe walishambuliwa kutokana na kile kilichodaiwa
kwamba wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM bungeni.
Habari zilidai kwamba waliowashambulia wabunge hao
ni wenzao, Saidi Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera), huku
wakitetewa na Beatrice Shellukindo (Kilindi) na Peter Serukamba (Kigoma
Mjini) ambao walikaririwa wakisema kwa nyakati tofauti kwamba
hawajakosea chochote kwani wanaeleza hali halisi ilivyo.
Baada ya mjadala huo, Pinda alikaririwa
akimwelekeza Katibu wa Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kumwandikia
barua Katibu Mkuu wa CCM, Kinana kuhusu suala hilo ili liwe ajenda
watakapokutana na Rais Kikwete.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba huenda hoja hiyo
ikakosa nguvu kutokana na msimamo wa sasa wa Kinana ambaye anawaona
wabunge wa CCM kama ni wapole, hali inayosababisha wale wa vyama vya
upinzani hasa Chadema kupata nguvu.
Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwamba Rais
Kikwete atakuwa na wakati mgumu wa ama kukubaliana na hoja za wale
wanaokosoa wenzao kwa kuikosoa Serikali au kuegemea upande wa Kinana
ambaye kimsingi anaunga mkono ukosoaji unaofanywa na wabunge.
Harufu ya kile kinachodaiwa kuwa ni maandalizi kwa
ajili ya mkutano huo ilianza kunukia jana pale Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda alipomtaka Lugola kuwasilisha ushahidi wa majina ya mawaziri
aliodai kwamba wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ili
ayafikishe kwa Rais Kikwete kwa hatua zaidi.
“Kila mtu anatakiwa aipime kauli yake kabla
hajaitamka, kama Lugola ana ushahidi aulete mbele ya Bunge na
tutayapeleka kwa Rais,” alisema Pinda wakati akijibu swali la Mbunge wa
Tumbe, Rashid Ally Abdallah aliyesema anaamini hakuna waziri
anayejihusisha na biashara hiyo kwani mchakato wa kuwapata hufanywa kwa
umakini wa hali ya juu.
Abdallah alikuwa akirejea kauli iliyotolewa na
Lugola mwezi uliopita kwamba atawasilisha bungeni majina ya watendaji wa
Serikali wanaopokea rushwa ili kuficha majina ya mawaziri
wanaojihusisha na dawa za kulevya na kwamba kauli hiyo ni nzito
inayolidhalilisha Bunge.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment