ZITO AWASHA MOTO BUNGENI
WABUNGE wa CHADEMA; Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na John
Mnyika (Ubungo), wamewachochea wabunge wenzao wasihudhurie semina
iliyoandaliwa leo na Wizara ya Nishati na Madini.
Sababu waliyoitoa wabunge hao juu ya ushawishi huo ni kuwa serikali
imeanza ugawaji wa vitalu vipya vya mafuta na gesi kwenye bahari kuu na
Ziwa Tanganyika Kaskazini.
Hata hivyo, hatua hiyo imeonekana kuwagawa wabunge, ambapo baadhi wamepinga na wengine kuunga mkono.
Kupitia taarifa zao kwa vyombo vya habari walizozituma kwa nyakati
tofauti, Zitto na Mnyika wamepinga uamuzi wa serikali wa kuanza mzunguko
wa nne wa ugawaji wa leseni za utafutaji na ugunduzi wa gesi nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto ameonesha kushangazwa
na uamuzi huo wa serikali, kwani Tanzania bado haijawa na sera ya gesi
asilia na kwamba ndiyo kwanza wabunge wamepewa rasimu ya sera hiyo kwa
ajili ya kutoa maoni yao.
“Kesho Jumamosi wabunge tumealikwa kwenye semina kuhusu sera ya gesi
asilia. Tumegawiwa tayari nakala zetu, tena zipo kwenye lugha ya
kimombo,” alisema Zitto na kuongeza;
“Jambo la kushangaza ni kwamba wakati sera ya gesi asilia ipo kwenye
rasimu na ndiyo kwanza wabunge tumeletewa kutoa maoni, serikali tayari
imetangaza tena kugawa vitalu vya mafuta na gesi kwenye bahari kuu na
Ziwa Tanganyika Kaskazini.”
Pia katika taarifa hiyo Zitto ameelezea kushangazwa na hatua hiyo ya
serikali ambayo alisema inakwenda kinyume cha maamuzi ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozuia ugawaji mpya wa vitalu hadi
sera ya gesi asilia na sheria ya gesi vikamilike.
“Haraka hii ya serikali kugawa vitalu bila sera wala sheria inatoka
wapi? Nitashangaa sana wabunge kukimbilia posho za semina hii na
kuhalalisha maamuzi yasiyozingatia maslahi ya taifa kwa vizazi vya sasa
na vijavyo,” alisisitiza Zitto.
Zitto amewataka wabunge na wananchi kuupinga uamuzi huo wa serikali.
“Uamuzi wa kugawa vitalu vipya bila kwanza kuwepo kwa sera na sheria
mpya unapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Tafuta mbunge wako, mwambie
asikubali maamuzi haya ya serikali. Tumalize kwanza sera na sheria ndiyo
tugawe vitalu vipya. Gesi sio viazi, haiozi,” imesisitiza taarifa hiyo.
Naye Mnyika amesema kuwa si sahihi kwa serikali kuanza kutoa leseni
mpya za utafutaji na ugunduzi wa gesi nchini wakati taifa likiwa bado
linaendelea na mchakato wa katiba mpya.
“Taifa letu lipo kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya huku kukiwa
na kumbukumbu chungu za miaka zaidi ya 20 ya kupata hasara kubwa baada
ya kufungua mianya ya ufisadi na unyonywaji katika sekta ya uchimbaji
madini na rasilimali zingine muhimu,” ilisema taarifa yake kwa vyombo
vya habari.
Taarifa hiyo inapendekeza kuwa ingekuwa vema kwa serikali kusubiri
kwanza kukamilika kwa mchakato wa kupata katiba mpya ili kuhakikisha
kuwa udhaifu wa kikatiba, kisera, kisheria, kiuongozi na kitaasisi
umerekebishwa.
“Hivyo, badala ya kukimbilia kutangaza mzunguko mwingine huku tayari
taifa likiwa kwenye lindi la ufisadi na unyonyaji kupitia mikataba
iliyotangulia ya gesi asili; nguvu za wananchi zielekezwe katika kutaka
katiba mpya kuwa na vifungu vitakavyolinda rasilimali muhimu kama
mafuta, gesi madini na mali asili nyingine,” imesisitiza taarifa hiyo.
Hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC) imetoa taarifa ya kuzinduliwa kwa mzunguko
wa nne wa utoaji leseni za utafiti na ugunduzi wa gesi asilia nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari, na
tovuti ya TPDC ni kwamba utoaji leseni za utafiti na uzinduzi huo
utaanza mwezi Oktoba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, leseni zitakazotolewa zitahusisha utafiti
katika Ziwa Tanganyika lililopo magharibi mwa Tanzania, na ndani ya kina
kirefu cha maji ya Bahari ya Hindi kwa upande wa mashariki na kusini
mwa bahari hiyo.
Itakumbukwa kwamba hapo awali wizara ilitangaza kutokuingia mikataba
yoyote ya utafiti na uvumbuzi wa gesi asilia hadi pale sera ya mafuta na
gesi itakapokuwa tayari.
Msimamo wa CHADEMA kuhusu sekta ya mafuta na gesi uko wazi ambapo
inataka kwanza kuandaliwa kwa sera na sheria ya mafuta na gesi kabla ya
kuingia mikataba mipya ya utafutaji na ugunduzi wa nishati hizo.
Baadhi ya wabunge wamelidokeza Tanzania Daima kuwa kutohudhuria semina
hiyo ni kujikosesha fursa ya kujua kitakachowasilishwa na serikali.
Walibainisha kuwa wasipohudhuria semina hiyo hawatakuwa na uwanja mpana wa kupinga kile wanachokiona si sawa.
Waziri Muhongo anena
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema Tanzania inatumia sheria ya gesi asilia na mafuta ya mwaka 1980.
“Watu waache kupotosha..., si kweli kuwapo maamuzi ya Bunge ya
kutogawa vitalu vipya vya utafutaji wa gesi asilia na mafuta bali
kinachofanyika ni kuiboresha sera na sheria ya gesi asilia ili
kuitengenisha na mafuta,” alisema.
Alisema kuwa utafutaji huo haukuanza leo na kwamba anayegundua ndiye anatafuta sana.
Profesa alifafanua kuwa kwa sasa wanafanya maboresho ya kulijenga upya Shirika la Mafuta (TPDC) lililoanzishwa mwaka 1969.
“Hawa Watanzania wanaotoa taarifa za uongo kwenye mitandano na kutaka
kupotosha watu, wanaikosesha nchi maendeleo. Maana hayo makampuni ya
mafuta wanayoyapiga vita ndiyo hayo yanatafuta mafuta Msumbiji na Kenya,
kwanini sisi tukatae?” alihoji.
Alisema kuwa kama nchi isingekuwa na sera ya gesi na mafuta hata hao
wawekezaji wasingekubali kuwekeza kwenye nchi ambayo haina sheria.
Waziri Muhongo alisema kuwa leo watafanya semina kwa wabunge wote
mjini hapa kuhusu sera hiyo ya gesi, na hivyo kuwataka wote wenye
dukuduku walete hoja zao wapate ufafanuzi.
No comments:
Post a Comment