WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Lupata, inayomilikiwa na
Jumuiya ya Wazazi (CCM) wilayani Rungwe wamefanya vurugu na
kuliteketeza kwa moto bweni la wavulana wakipinga kitendo cha wanafunzi
wenzao watatu kusimamishwa masomo kwa utovu wa nidhamu.
Taarifa za tukio hilo zimetolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Mbeya, Diwani Athuman, na kwamba vurugu hizo zilitokea juzi majira ya
saa 2:00 usiku baada ya wanafunzi waliosimamishwa masomo kuwahamasisha
wenzao kupinga adhabu hiyo.
Kamanda Diwani alisema tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa mali za shule hiyo ingawa moto huo haukusababisha madhara.
Alisema chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na wafunzi hao; Joseph
Robert (18) mwanafunzi wa kidato cha nne, Mwita Chacha (17) mwanafunzi
wa kidato cha tatu wote wakazi wa Kitunda, Dar es Salaam kusimamishwa
masomo kwa utovu wa nidhamu.
Alisema mwanafunzi mwingine anayehusika katika kuhamasisha wenzao
kufanya vurugu hizo ni Daniel David (18) anayesoma kidato cha tatu na
mkazi wa Ipinda, wilayani Kyela.
Kamanada huyo alisema bweni lililoteketea kwa moto lilikuwa na wanafunzi zaidi ya 50 ambao waligoma kuwaunga mkono wenzao.
Kutokana na tukio hilo, alisema wanafunzi 15 wakiwamo waliosimamishwa
masomo wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
|
No comments:
Post a Comment