VITENDO vya kigaidi vilivyolikumba taifa hivi karibuni, vimeanza kulitia hofu Bunge na kuamua kuchukua tahadhari.
Taarifa ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah aliyosomwa bungeni juzi mara mbili na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu iliwataka wabunge kuanzia sasa wawe wanaegesha magari yao ndani ya uzio wa Bunge badala ya kuyaegesha nje kama ilivyozoeleka.
“Waheshimiwa wabunge kuna tangazo muhimu hapa linatoka kwa Katibu wa Bunge, linasema kuwa kutokana na tishio la vitendo vya kigaidi vinavyoendelea nchini mwetu, kuanzia sasa magari ya wabunge wote yawe yanaegeshwa ndani ya uzio kwenye maegesho na si nje ya uzio wa Bunge kama baadhi wanavyofanya,” alisema.
Zungu aliongeza kuwa kwa wale watakaotaka kuendelea kuegesha magari yao nje ya uzio, watapaswa kuyaegesha ng’ambo ya barabara ya Dodoma-Dar es Salaam mkabala na Ukumbi wa Bunge.
Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema kuwa hakuna taarifa yoyote ya vitisho waliyoipokea isipokuwa wanachukua tahadhari mapema ya kujilinda kutokana na taasisi hiyo kuwa muhimu.
Joel alisema kuwa wanafanya hivyo mapema badala ya kungoja tukio litokee na watu kupoteza maisha ndipo wachukue hatua.
No comments:
Post a Comment