Pages

Friday, May 17, 2013

RPC Kamhanda alikoroga tena • Adai Mahakama Kuu imeiba kielelezo cha bangi

KAMANDA wa polisi mkoa wa Iringa (RPC), Michael Kamhanda, ameingia matatani tena baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, kusema kuwa ametoa taarifa ya uongo kwamba mtumishi wa mahakama hiyo, Lwitiko Minga, ameiba kielelezo cha bangi, kilichowasilishwa kama ushahidi.

Kamuhanda ambaye bado anakabiliwa na shinikizo la kutaka afikishwe mahakamani kutokana na mauaji ya mwandishi wa habari, Daud Mwangozi, juzi aliilipua mahakama hiyo kwamba imeiba kielelezo hicho na kukiuza tena mitaani kinyume cha sheria.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Kamhanda alidai kuwa jeshi la polisi mkoani humo linamshikilia mtumishi huyo kwa madai ya kuiba bangi hiyo iliyofikishwa mahakamani hapo kama kielelezo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kujibu madai ya Kamuhanda, Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Godfrey Isaya, alisema mahakama hiyo imesikitishwa sana na taarifa hiyo aliyoiita kuwa ni ya uongo na uzushi.

“Taarifa ya kamanda wa polisi kuwa bangi imeibiwa mahakamani si ya kweli na imelenga kuichafua mahakama hiyo kwani hatujaibiwa kielelezo hicho,” alisema Isaya.

Alisema kuwa jeshi la polisi limeupotosha umma kwa kutoa taarifa ya uogo bila kufanya uchunguzi.

Isaya alisema kama kielelezo hicho kingeibiwa, mahakama ambayo kimsingi ndio mlalamikaji, ilipaswa kwenda kufungua kesi polisi.

“Tunakanusha vikali kuwepo kwa upotevu wa kielelezo cha bangi katika mahakama hii ‘Exhitibit Room’ haijavunjwa iko vilevile .....,” alisema Isaya.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Isaya alisema katika kesi ya jinai namba 24/2012, mahakama hiyo ilipokea kielelezo P.3 ambacho ni bangi viroba vinane na amri ya mahakama ya kuteketeza bangi hiyo ilitolewa Februari 13, mwaka huu.

Alisema bangi hiyo iliteketezwa chini ya uangalizi wa ofisa wa jeshi la polisi na kesi hiyo ilimalizika Aprili 13 mwaka huu na mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

“Tunatoa wito kwa jeshi la polisi Iringa kufanya uchunguzi wa kina kubaini bangi hiyo imepatikana wapi kwani sisi kama mahakama hatujapata kuibiwa bangi katika mazingira yoyote na kama tukio hili lingekuwepo basi taarifa zingeripotiwa polisi,” alisisitiza.

“Tunalishauri jeshi la polisi kufanya utafiti wa kina kuhusu suala hili kabla ya kutoa taarifa katika vyombo vya habari na linapaswa kuja kuwahoji wahusika na kuchunguza suala hilo kabla ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari,” alisisitiza.

Katika mkutano wake na vyombo vya habari jana, Kamanda Kamuhanda alisema kielelezo hicho cha bangi kiliibwa Februari 14 mwaka huu.

Alimtaja mtuhumiwa wa wizi huo kuwa ni Lwitiko Lusekelo Minga ambaye ni mlinzi wa mahakama ya wilaya ya Iringa, ambaye anadaiwa kuiba bangi hiyo yenye uzito wa kilo 371.2.

Kamhanda alisema bangi hiyo ilikamatwa eneo la Frelimo mikononi mwa Juma Nzowa ambaye alipohojiwa alimtaja Lwitiko kuwa ndiye aliyemuuzia kielelezo hicho cha mahakama.

Alisema awali bangi hiyo ilikamatwa wilaya ya Kilolo na kufikishwa mahakamani kama ushahidi na ndipo ilipoibiwa tena.

Kamanda Kamhanda alisema imekuwa kawaida kwa watumishi wasio waaminifu wa mahakama kuiba vielelezo kama dawa za kulevya vinapofikishwa mahakamani na kisha kuibiwa vikiwa mikononi mwa mahakama na kurudishwa tena mitaani, hali inayofanya kazi yao kuwa ngumu.

 

Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment