Rais Jakaya Kikwete akipewa maelezo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Adam Mayingu (kulia)
alipotembelea banda la mfuko huko wakati wa ufungaji wa maonyesha ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Sakata
la kuanzishwa kwa malipo ya pensheni kwa wazee bado ni giza nene baada
ya Rais Jakaya Kikwete kutaka hatua hiyo isifanywe kwa kukurupuka.
Aidha, ameahidi kwamba Serikali italipa kiasi cha Sh6 trilioni inazodaiwa na Mfuko wa Hifadi wa PSPF.
Akizungumza jana wakati wa kilele cha Siku ya
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Mjini
Dodoma, Rais Kikwete alisema:
“Nakuagiza Waziri Kabaka, kuwa anzeni sasa
kufikiria namna ya kuwalipa wazee pensheni, lakini msikurupuke kufanya
hivyo kwani ni lazima kujiridhisha kwanza kabla ya kuanza kutoa mafao
hayo maana mtaaibika.”
Aliongeza: “Nawaomba msiahidi kwa watu kitu
msichoweza kukifanya na kuwa endelevu kwani mtaaibika, hivyo jipangeni
vizuri kabla ya kuanza kutoa, waelezeni ukweli wazee.”
Rais aliwataka wataalamu kujifunza kutoka kwa nchi
nyingine zilizofanikiwa akieleza kuwa wazee hawakuwahi kuchangia, hivyo
kutoa malipo kwa wazee ambao ni zaidi ya milioni mbili nchini ni kazi
kubwa.
Kwa upande mwingine Rais aliwatoa wasiwasi
Watanzania kuwa mifuko ya hifadhi haitafilisika, huku akiahidi kuwa
Serikali italipa deni lote inalodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ili
kuhakikisha inafanya kazi yao iliyokusudiwa ikiwemo kuwalipa wastaafu.,
“Si kweli kuwa mfuko wa PSPF una hali mbaya kiasi
cha kushindwa kujiendesha na kuitwa mahututi, bali mfuko huo unaidai
Serikali kiasi cha fedha Sh6 trilioni na fedha hizo zitalipwa,”alisema
Kikwete.
Alirudia ahadi yake kuwa Serikali italipa deni
hilo na lile la Sh10 bilioni ambalo LAPF inaidai ili Serikali
isiwatapeli wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment