Kauli ya
Serikali iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa
kidato cha nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, imeibua utata
baada ya taarifa kadhaa kuonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.Taarifa ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3,
mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi ilisema Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya
mabadiliko ya mfumo bila kushirikisha wadau.
“Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata
alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kwa
kutegemeana na hali ya ufaulu wa mwanafunzi... lakini mwaka 2012
lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (fixed
grade ranges).”
“Tume imebaini kwamba, pamoja na mfumo huo
kuandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na
maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
“Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa
kuzingatia kuwa pamoja na kwamba sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu
kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya
kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya
matokeo ya mtihani lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa,
ufundishaji na mitihani.”
Kwa mujibu wa vielelezo vilivyochapishwa na Gazeti
la Wiki la Jamhuri, mfumo huo ulipitishwa na Serikali kupitia Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa, kikao kilichokutana
na kujadili mapendekezo ya Necta ya kubadili mfumo huo kiliongozwa na
Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa na Katibu wake alikuwa Naibu Waziri
wa Elimu, Philip Mulugo.
Muhtasari wa kikao hicho unaonyesha wajumbe wa
mkutano huo walikuwa ni pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Selestine Gesimba, Kamishna wa Elimu, Profesa Eustell Bhalalusesa,
Paulina K Mkonongo, Marystella Wassena, T.E. Temu, Katibu Mtendaji wa
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus Nkwera, Bunyanzu
Ntmabi, H.A Lihawa wote wakiwa wajumbe kwa upande wa Wizara.
Kutoka Necta wajumbe walikuwa ni Dk C.E Msonde,
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Bodi
ya Necta, Profesa Rwekaza Mukandara pamoja na Profesa Sifuni Mchome,
ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Aidha, Gesimba alimwandikia barua Katibu Mtendaji
wa Necta yenye kumbukumbu namba CAC.109/437/01N Desemba 12 mwaka jana
akiliagiza kutumia mfumo mpya wa kukokotoa alama za mitihani ya kidato
cha nne na sita.
“Tafadhali rejea kikao kilichofanyika tarehe
10/12/2012 katika ukumbi wa mikutano wa wizara kuhusu somo tajwa hapo
juu (Maagizo ya kuhusu utaratibu wa matumizi ya viwango vya ufaulu
katika mitihani ya kidato cha nne na sita).
“Viwango vya ufaulu vilivyopendekezwa na Baraza la
Mitihani la Tanzania vitumike kwa mitihani ya Kidato cha Nne 2012 na
Kidato cha Sita kwa mwaka 2012 tu.
No comments:
Post a Comment