Pages

Thursday, May 16, 2013

MABAKI YA MWANAMKE YAKUTWA JIRANI NA MAGEREZA


MABAKI ya mwili  wa mwanamke  anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30 ambaye jina lake halikufahamika, yamekutwa  eneo la Magereza, Kata  ya Miyomboni Kitanzini, Manispaa ya  Iringa.


Mabaki hayo  yalikutwa majira ya saa 6:00 mchana, juzikati yakiwa yamesambaratika kutokana na kuoza.

 Walioyakuta ni maofisa wa magereza ambao walikuwa katika  eneo hilo na wafungwa  wakikata miti kwa ajili ya  kuni.

Wakizungumza na Amani, baadhi ya  mashuhuda walidai kuwa mwanamke  huyo inaonekana siku ya kifo chake alikuwa amevaa suruali nyeusi, kilemba cha kitenge chenye madoa mekundu, njano, meusi na meupe pamoja na skafu ya rangi nyeupe na nyeusi.

Mashuhuda hao walidai kuwa  mwanamke huyo alipoteza maisha kwa zaidi ya wiki  mbili nyuma kutokana na mabaki hayo kuharibika kupita kiasi na kukauka.

Mazingira ya kifo cha mwanamke huyo yalionesha utata  kwa kuwa hata polisi  waliofika eneo la tukio, walikiri kutokuwepo kwa taarifa yoyote ya mtu  kupotea na kwamba  inawezekana alivamiwa ama alikufa kwa matatizo yake au alikuwa akitoka hospitali ambayo ipo jirani na eneo hilo. 

Mabaki ya  mwili  huo yalichukuliwa na polisi na kuhifadhiwa katika Chumba cha Maiti cha Nina Marwaha cha Hospitali ya Rufaa Mkoa  wa Iringa.

chanzo:.globalpublishers

No comments:

Post a Comment