RASIMU ya Sera ya Elimu na Mafunzo
nchini inapendekeza kuunganisha elimu ya msingi na sekondari ya kawaida
ya sasa ili kuunda elimu-msingi itakayotolewa kwa kipindi cha miaka 10
kuanzia mwaka 2018, imefahamika.
Rasimu ya kwanza ya Sera hiyo
imeshakamilika na sasa wadau mbalimbali wanatoa mapendekezo yao
kuiboresha, kabla ya kupelekwa bungeni ili kutungiwa sheria.
Aidha, mikakati hiyo itakayotekelezwa
ni kuhuisha muundo na utaratibu mpya wa elimu na mafunzo kwa
kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na mitano anapitia
elimu ya awali kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya kujiunga
na elimu-msingi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo alithibitisha kwa gazeti hili wiki hii mjini hapa
kuhusu kukamilika kwa rasimu ya kwanza ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya
mwaka 2013.
“Ni kweli Sera hiyo imekamilika baada
ya kuandaliwa kwa miaka mitatu. Imepita kwa wadau mbalimbali,
mashuleni, vyuoni na katika taasisi mbalimbali nchini ambao wametoa
maoni yao. “Jumapili (kesho) tunatarajia kuwa waheshimiwa wabunge nao
watapata fursa ya kuijadili na kutoa maoni yao katika semina
iliyoandaliwa maalumu kwao,” alisema Mulugo katika Viwanja vya Bunge.
Alisema baada ya maoni hao ya
wabunge, watapeleka Rasimu hiyo kwa mamlaka husika kwa ajili ya andiko
la mwisho kabla ya kupelekwa katika Bunge lijalo ili itungwe sheria
kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo.
Hata hivyo, semina hiyo huenda
isifanyike kesho kutokana na kuingiliana na ratiba nyingine, kwani
wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakuwa na mkutano na Mwenyekiti
wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwenye Ukumbi wa White House mjini
hapa.
Wiki moja iliyopita, wakati akiongoza
kikao, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwaambia wabunge kuwa makabrasha
waliyokuwa wakipewa na wahudumu ni kuhusu Sera ya Elimu na hivyo waende
wakayasome, kwani kuna siku wataijadili.
Kwa mujibu wa rasimu, mambo mengine
yanayotarajiwa kutekelezwa na Sera ni kuhuisha mitaala ya sasa ya elimu
ili ikidhi muundo mpya wa elimu na mafunzo, kuhuisha sheria na taratibu
mbalimbali za utoaji elimu ili ziendane na muundo mpya wa elimu-msingi.
Kuimarisha mfumo wa usimamizi,
ithibati na udhibiti wa utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi
mbalimbali ili kukidhi malengo na muundo mpya wa elimu-msingi.
Nyingine ni kuongeza ubora wa
miundombinu katika shule za sasa za msingi ili kukidhi mahitaji na
malengo ya elimu-msingi ikiwa ni pamoja na kuongeza madarasa ya
elimu-msingi katika kila shule ya msingi ya sasa, kujenga maabara za
sayansi na maktaba katika kila shule ya elimu-msingi.
“Kutenga rasilimali fedha za kutosha
kwa ajili ya nyenzo, vifaa na zana za kufundishia na kujifunzia, vitabu
vya kiada na ziada, maandiko, machapisho ya maktaba pamoja na vifaa vya
maabara,” ilieleza rasimi hiyo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Kuimarisha matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza katika ngazi ya
elimu – msingi kama lugha za kujifunzia na kuwasiliana.
Kuweka utaratibu utakaohakikisha kuwa
wanafunzi wanaomaliza elimu na mafunzo ngazi husika kwa ufanisi na wale
wanaokatisha masomo au mafunzo yao kwa sababu mbalimbali, wanaendelea
na kuhitimu masomo au mafunzo yao katika mfumo rasmi wa elimu na
mafunzo. Jambo jingine litakalotekelezwa ni kutoa elimu kwa umma kuhusu
madhumuni, malengo na matarajio ya Sera mpya ya Elimu na Mafunzo.
Rasimu ilieleza kuwa mambo chanya
yanayotarajiwa kupatikana baada ya mkakati kutekelezwa ni kuwepo kwa
elimu ya awali ya lazima kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya
kujiunga na elimu msingi, kuwepo kwa elimu msingi ya miaka 10 kuanzia
darasa la kwanza hadi kidato cha nne cha sasa kwa watoto wote wenye rika
la kwenda shule.
Matokeo mengine ni kuwepo kwa mfumo
nyumbufu, miundo na taratibu za kujiendeleza katika mikondo anuai ya
kitaalamu na kitaaluma, kuwepo kwa elimu na mafunzo yenye viwango, ubora
na sifa zinazotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.
“Kuwepo kwa fursa mbalimbali za elimu
na mafunzo zinazokidhi mahitaji ya wananchi na ya nchi kiuchumi,
kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
“Kuwepo kwa ugharimiaji endelevu wa
elimu na mafunzo na kuwepo kwa mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia
masuala mtambuka,” ilifafanua Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo.
Kuhusu elimu ya awali, ilieleza kuwa
mkakati ni kuweka vigezo, viwango na taratibu ili elimu ya awali iwe ya
lazima na itolewe katika kila shule ya elimu – msingi, na kuwa sheria,
miongozo na taratibu kuhusu elimu hiyo lazima kuwekwa na kutekelezwa
ifikapo mwaka 2018.
Katika elimu msingi, ni kuwa ya
lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na kutolewa kwa
miaka 10 na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne
hadi sita kulingana na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.
Shabaha katika eneo hili ni sheria na
miongozo kuhusu elimu-msingi kuwekwa na kutekelezwa ifikapo mwaka 2016,
mpango wa utekelezaji wa utoaji wa elimu-msingi kuwepo ifikapo mwaka
2018 na elimu-msingi kutolewa ifikapo 2018.
Kwa mujibu wa dibaji ya Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Sera mpya imeandaliwa
na Serikali kwa kushirikiana na wadau ikitilia maanani mafanikio
yaliyoletwa na Sera zilizotangulia na kulifanya Taifa kupiga hatua
katika nyanja za elimu na mafunzo.
“Sera kuu zilikuwa ni Sera ya Elimu
na Mafunzo 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo 1996 na Sera ya
Taifa ya Elimu ya Juu 1999 ambazo zilitekelewa sambamba na sera nyingine
ambazo zinaigusa sekta ya elimu na mafunzo kama vile Sera ya Sayansi na
Teknolojia 1996, Sera ya Habari na Utangazaji 2003, Sera ya Ubia kati
ya Sekta ya Umma na ya Binafsi 2009 pamoja na nyingine za aina hiyo,”
alisema Dk Kawambwa.
Source:Zeddylicious blog
No comments:
Post a Comment