Imebainika
kuwa soda imepigwa marufuku kutumiwa na watoto walio na umri chini ya
miaka 12 na walio shuleni katika baadhi ya mataifa ya Ulaya na Marekani,
kutokana na madhara ya kiafya yanayosababishwa na kinywaji hicho,
limeandikwa gazeti la Mtanzania la leo
Taarifa
zilizotolewa na Shirika la Habari la The Press Television Technology
Advertising and Branding (Adweek) zinazonukuu taarifa ya kampuni moja
kubwa duniani inayozalisha kinywaji aina ya soda, imeamua kupambana na
unene (obesity), unaosababishwa na unywaji wa soda kwa kuondoa matangazo
ya vinywaji vyake kwenye vyombo vya habari.
Kampuni hiyo kupitia
taarifa yake hiyo iliyotolewa katika moja ya sherehe zake, ilieleza
kuwa lengo la kuondoa matangazo hayo ni kuwanusuru watoto wadogo na
matumizi ya vinywaji aina ya soda vilivyobainika kuwa na madhara katika
mwili wa binadamu.
Nchini Marekani, tayari imekwishapitishwa
sheria inayokataza watoto walio na umri wa chini ya miaka 12, kunywa
kinywaji aina ya soda.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, alieleza kuwa
mipango ya mbeleni ya kampuni yake ni kutengeneza kinywaji hicho kikiwa
na kiwango kidogo cha Kalori na kubuni kinywaji cha aina hiyo ambacho
kitakuwa hakina Kalori.
Alisema mipango hiyo itatekelezwa duniani
kote ambako kinywaji cha aina ya soda kinatengenezwa na nchini Marekani
tayari imekwishaanza kutekelezwa.
Aidha, Kampuni hiyo imeahidi
kuweka wazi virutubisho vyote vinavyotumika kutengeneza bidhaa zake na
kuahidi kutoa misaada ya hali na mali kwa nchi zote 200 duniani ambako
kinywaji cha soda kinauzwa.
Mbali na Marekani, kinywaji cha aina
ya Soda kimekwishapigwa marufuku shuleni katika nchi za Uingereza,
Ufaransa na katika majimbo ya Los Angeles, Philadelphia na Miami nchini
Marekani na kwa watu wazima matumizi yake yanaelekezwa kuwa ya kiwango
kidogo sana.
Vyombo vya habari vya nchini New Zealand, mwezi
Machi mwaka huu viliripoti kuwa mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la
Natasha Harris (31), alifariki kutokana na unywaji wa soda nyingi.
Shirika
la habari la AFP la Ufaransa, liliripoti tukio hilo kwa kueleza kuwa
Natasha alikuwa akinywa soda nyingi kila siku, jambo ambalo liligeuka
kuwa sehemu ya maisha yake kwa kipindi cha miaka mingi.
Kwamba
familia ilikuwa ikimuita teja wa soda, baada ya meno yake kuoza kwa
sababu ya kunywa soda, alijifungua mtoto ambaye hakuwa na fizi jambo
ambalo liligundulika baadaye kuwa lilisababishwa na matumizi makubwa ya
kinywaji hicho.
“Tumegundua kwamba, kwa kuzingatia ushahidi
uliopo, kama sio unywaji wa soda uliopitiliza, Natasha Harris asingekufa
katika muda ule na katika hali alivyokufa
“Ripoti ya Daktari
aliyechunguza maiti yake (Pathologia), iligundua kwamba ini lake
lilipanuka sana, likawa na mrundiko mkubwa wa mafuta kutokana na kula
sukari kwa wingi. Kuwepo kwa madini aina ya ‘potasiam’ kwa kiwango
kidogo sana kwenye damu yake, pia kulitokana na unywaji wa soda.”
Taarifa ya kitabibu katika Hospitali aliyofia nchini New Zealand
ilieleza.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi zilizo
kwenye mitandao ya wanasayansi waliobobea duniani, unywaji wa soda
humpumbaza mtumiaji na kumsahaulisha kula vyakula vyenye madini muhimu
mwilini.
Moja ya andishi linalotahadharisha utumiaji wa kinywaji
cha soda na kukitaja kuwa cha hatari kwa matumuzi ya binadamu, ni Jack
Winkler, Profesa wa sera za lishe katika Chuo Kikuu cha Metropolitan
nchini London, linaloeleza kuwa Soda ni bidhaa ya kishetani inayoua
binadamu taratibu baada ya kinywaji hicho kumzalishia magonjwa mengi
mwilini yanayomfanya kuwa tegemezi wa dawa.
Wakati msomi huyo
akieleza hayo katika utafiti wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) Dk. Raymond Wigenge, amelekeza soda siyo kinywaji hatari kwa
matumizi ya binadamu kwa sababu kinatumiwa na mamilioni ya watu duniani
kote.
Dk. Wigenge alisema pamoja na changamoto zilizopo katika kinywaji hicho, taasisi yake haipingi uwepo wa kinywaji hicho sokoni.
“Soda
haina shida kwa binadamu na hata mkiendelea kuandika suala hili, sisi
tutaendelea kuueleza umma kwamba waendelee kupata kinywaji, hivyo kama
ambavyo tumekuwa tukifanya,” alisema.
Alipoulizwa kama
anakubaliana na tafiti za wanasayansi bingwa wa magonjwa ya binadamu
walioeleza katika tafiti zao kuwa unywaji wa soda una madhara katika
mwili wa binadamu, alisema hizo ni changamoto za kawaida, kwa sababu
madhara yaliyomo kwenye soda hayamuathiri mtu mara moja bali huchukua
muda mrefu.
Wakati Dk. Wigenge akieleza msimamo wake kuhusu
kinywaji aina ya soda, nchini Mexico, taasisi ya El Poder del Consumidor
inayojihusisha na kutetea walaji, inashinikiza Serikali ya nchi hiyo
kuzilazimisha kampuni za soda kuorodhesha madini na chembechembe zote za
kemikali zinazotumika kutengeneza kinywaji hicho.
Mkurugenzi wa
taasisi hiyo, Alejandro Calvillo, amekaririwa na vyombo vya habari vya
nchi hiyo akieleza kuwa unywaji wa soda ni hatari na hilo
limethibitishwa na wataalamu wa afya duniani kuwa soda ni sumu mbaya,
inauwa taratibu.
Tafiti mbalimbali za wanasayansi zinaeleza kuwa
soda ina asidi aina ya ‘phosphoric’ yenye uwezo wa kuvuruga madini ya
‘calcium’ yaliyoko mwilini na kusababisha mifupa na meno kudhoofika.
Aidha,
asidi aina ya ‘phosphoric’ huvuruga asidi aina ya ‘hydrochloric’ iliyo
tumboni mwa binadamu na hivyo kuharibu mfumo wa kusaga chakula.
Viwanda
vya soda ndio watumiaji wakubwa wa sukari na wanasayansi wanasema
sukari hupandisha kiwango cha ‘insulin’ ambayo husababisha kasi ya
mzunguko wa damu, ugonjwa wa moyo, kupanda kwa ‘Cholesterol, kisukari,
kuzeeka mapema, ongezeko la uzito na maradhi mengine.
Aidha
inadaiwa kuwa viwanda vya soda pia hutumia dawa ya kulevya aina ya
kafeini. Wataalamu wanasema vinywaji vyenye kafeini, husababisha kupanda
kwa mapigo ya moyo, kasi ya mzunguko wa damu na matatizo ya kizazi.
No comments:
Post a Comment