Manusura wa jengo lililoporomoka nchini Bangladesh, Reshma Begum akiwa
katika picha ya pamoja na maofisa wa jeshi kwenye hospitali ya jeshi
mjini Dhaka, Bangladesh baada ya kuokolewa na kupatiwa huduma ya
kwanza, ambapo alieleza namna alivyonusurika.
Picha na AFP
Kwa ufupi
Japan mwaka 2004: Mtoto mwenye umri wa miaka
miwili aliokolewa akiwa hai baada ya siku nne, ndani ya gari lililokuwa
limezikwa ardhini.
Iran mwaka 2004: Mwanamke aliyekadiriwa
kuwa na umri wa miaka 90 aliokolewa akiwa hai baada ya siku nane za
kufukiwa na mabaki ya nyumba yake iliyobomoka kutokana na tetemeko la
ardhi.
Korea Kusini mwaka 1995: Mwanamke aliyekuwa amefukiwa na mabaki jengo la duka kwa siku 16, aliokolewa akiwa hai.
HABARI :
Msichana aliyenusurika baada ya kuishi kwa siku 17 chini ya
kifusi cha ghorofa lililoporomoka mjini Dhaka, Bangladesh, amesema
biskuti alizonunua kwa ajili ya kifungua kinywa akiwa kazini ndizo
zilimnusuru kufa kwa njaa.
Reshma Begum aliishangaza dunia baada ya kuokolewa
chini ya kifusi cha jengo hilo, lililoporomoka Aprili 24, mwaka huu na
kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.watu zaidi ya 2,500 waliokolewa
kati ya watu zaidi ya 3,000 ambao walikuwa wakifanya kazi ndani ya
jengo hilo la ghorofa nane.
Msichana huyo ambaye hakuwa na majeraha ya
kuhatarisha maisha yake, alisimulia mkasa wake kwamba aliishi kwa kula
biskuti na kunywa maji ya chupa yaliyodondoka kwenye eneo lake, bila
kufahamu yalikotoka.
Reshma (19) alisema siku ya ajali hiyo, aliamka
asubuhi kuwahi kazini bila kupata kifungua kinywa ambapo akiwa njiani
alinunua mabunda madogo manne ya biskuti ambazo angekula kabla ya kuanza
kazi.
Msichana huyo aliwasimulia mkasa huo wafanyakazi
wa hospitali na waokoaji kuwa aliishi kwa kula biskuti na kunywa maji ya
chupa, akiwa kwenye shimo lililokuwa na nafasi ya kumuwezesha kutembea.
Maji ya chupa aliyokuwa akitumia Reshma ni
miongoni mwa yaliyokuwa yakidondoshwa na waokoaji, kwenye kila shimo la
eneo la tukio.
Kwa mujibu wa taarifa, waokoaji walipewa maelekezo
ya kudondosha chupa za maji katika kila shimo watakaloona, kwa dhamira
ya kubahatisha huwenda chini ya shimo kuna binadamu walio hai na maji
hayo yalilenga kuwasaidia wakati juhudi za uokoaji zikiendelea.
Reshma ambaye anaishi peke yake katika chumba cha
kupanga kwenye kitongoji cha Savar, alisema wakati jengo hilo la ghorofa
nane lilipokuwa likiaguka alikuwa ghorofa ya tatu.
Alisema aliweza kushuka hadi ghorofa ya pili
ambako alinasa kwenye shimo kubwa. Alisema shimo hilo lilikuwa kubwa
kumuwezesha kutembea na kulikuwa na hewa ya kutosha.
Reshma alisema alipokwama kwenye shimo hilo pia
nywele zake zilibanwa na maporomoko ya mabaki ya jengo, ambapo
alilazimika kuzivuta hadi zikakatika ili awe huru.
Alisema licha ya kupiga kelele ya kuomba msaada
hakuweza kufanikiwa, na kwamba giza ndani ya shimo hilo lilimfanya
asijue usiku wala mchana.
No comments:
Post a Comment