Pages

Thursday, May 16, 2013

Pareso ahoji ujenzi barabara Karatu


 

MBUNGE wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (CHADEMA), ametaka kuelewa ni lini barabara ya Karatu njia panda-Mangola mpaka Bariadi katika Mkoa wa Simiyu itaunganishwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mbali na hilo, Pareso alitaka kuelewa ni kwanini zipo barabara ambazo zinatakiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini ujenzi huo unaonekana kusuasua na wakati mwingine kutojengwa kabisa.

“Mheshiniwa Naibu Spika kitendo cha kukosekana kwa barabara kunachangia kwa kiasi kikubwa wananchi kuendelea kuwa maskini hususan wale ambao wanazalisha mazao yao kwani wanashindwa kupeleka mazao sokoni na jambo ambalo linasababisha wafanyabiashara kununua mazao ya wakulima kwa bei ambazo wanazitaka wao,” alisema Pareso alipouliza swali bungeni jana.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema anatambua umuhimu wa barabara zote nchini, lakini ni lazima serikali ijenge barabara ambazo kwa sasa zipo katika mpango wa ujenzi wa barabara hizo.

Kuhusu barabara ya Karatu njia panda-Magola mpaka Bariadi, alisema serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo, hivyo itaangaliwa ni jinsi gani ya kuboreshwa zaidi.

“Natambua anachokieleza Mheshimiwa mbunge, najua zaidi umuhimu wa barabara hizo, hivyo ni lazima barabara zote zitajengwa.

“Tunajenga barabara za kuunganisha mikoa kwa mikoa nchi kwa nchi na kwa sasa kwa kiasi kikubwa mikoa mingi inaingilika kwa kiwango cha lami hivyo hata huko anakosema mbunge nako mambo yatakuwa mazuri,” alisema Dk. Magufuli.

 

Chanzo:Chadema blog

No comments:

Post a Comment