DC BUNDA KUTATUA MGOGORO WA ARDHI
MKUU wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Mirumbe, amewakutanisha
wakazi wa Kata ya Mikomariro wilayani Bunda na Silolisimba wilayani
Butiama wanaogombania mipaka ya ardhi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jana katika Kijiji cha
Mikomariro, Mirumbe alisema ameamua kuitisha kikao hicho kwa ajili ya
kuwakutanisha viongozi wa serikali za vijiji na viongozi wa kamati za
ulinzi na usalama, ili kuzungumzia suala hilo ambalo limekuwa likileta
hali ya kutoelewana.
Wakichangia maoni katika kikao hicho baadhi ya wananchi walidai
mgogoro huo ni wa muda mrefu na kwamba licha ya kusuluhishwa mara nyingi
mwafaka haujapatikana.
Mmoja wa wananchi, Alfred Mniko, alisema mwaka juzi walikaa kikao kati
ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda na Musoma na walipewa maelekezo kuhusu
mipaka hiyo, lakini wenzao wa Mikomariro hawakuridhika.
Naye Marabha Mwita alidai kuwa mwaka 1990 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mara Kanali mstaafu Issa Machibya alifika katika eneo hilo akawapa
ramani ya mipaka inayogombewa na kutaka kila upande uheshimu mipaka hiyo
lakini bado vurugu zimekuwa zikijitokeza.
“Mgogoro huu unaendeshwa kisiasa, lakini pia wataalamu wamechangia,
mfano wakurugenzi waliagizwa siku hiyo na mkuu wa mkoa waweke maboya
katika mipaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo, lakini hadi leo jambo
hilo halijatekelezwa,’’ alisema Juma Werema.
Akihitimisha kikao hicho, mkuu huyo wa wilaya alisema haoni sababu ya
wananchi hao kugombania mipaka na kwamba wanaofanya uharifu wa kuchomea
wenzao nyumba kwa kisingizio cha mipaka ya ardhi waache mara moja kwani
hilo ni kosa la jinai.
Aliwaagiza wenyeviti wa maeneo hayo kuitisha mikutano ili waweze kukaa
na wananchi wao kwa ajili ya kuzuia vitendo viovu wakati serikali
ikishughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment