VIVUTIO NYANDA ZA JUU KUSINI KUTANGAZWA
SERIKALI imesema ipo katika mchakato wa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Ofisa Habari wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Tulizo Kilaga, alisema mkoa mmojawapo ambao bado
hautambuliki katika sekta ya utalii ni Mbeya, ambayo ina vivutio vya
aina yake.
Alisema hawatangazi vivutio hivyo kwa watalii kutoka nje pekee, bali
hata Watanzania ambao ndio wamiliki wa rasilimali asili wanatakiwa
kuvifahamu na kuvitembelea.
Alisema Watanzania wakiwa na tabia ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini, watapanua ufahamu wa elimu na kuongeza uzalendo.
Alilitaja Ziwa Ngozi kama mojawapo ya kivutio kikubwa ambacho si tu kinavutia kutembelea, bali pia kina historia ya pekee.
Tulizo alisema ziwa hilo lililopo kati ya Wilaya ya Mbeya na Rungwe, limezungukwa na milima, ukiwemo Mlima Ngozi.
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa waongozaji wageni
wanaofika katika eneo hilo, Said Jaffar, alisema wamekuwa wakifaidika na
ziwa hilo, ambapo pia ni sehemu ya ajira kwa vijana waishio katika eneo
hilo.
“Msimu wa kiangazi, huwa tunapata wageni wengi hasa wanafunzi, ila
natumai likitangazwa vizuri, idadi ya watalii itaongezeka,” alisema.
Wakazi wa eneo ilo walisema ziwa hilo limekuwa halijai maji wala kupungua kwa majira yote ya mwaka.
No comments:
Post a Comment