MAMA PINDA: Tuombe Yasitokee Mabomu Mengine
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amesema Watanzania wote kwa pamoja
wana kila sababu ya kujinyenyekeza mbele za Mungu na kuendelea kuomba
ili pasitokee tena ulipuaji wa mabomu kama lile la Arusha.
Ametoa wito huo Alhamisi, Mei 16, 2013 alipokuwa akiongea na Katibu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padre Prosper Lyimo wakati
alipokwenda kwenye nyumba ya Askofu ili kuwapa pole kwa maafa
yaliyowapata waumini wa Parokia teule ya Olasiti jijini Arusha, Mei 5
mwaka huu.
Padre Lyimo alimpokea Mama Pinda kwa niaba ya Askofu Mkuu wa jimbo
hilo, Mhashamu Josephat Lebulu ambaye alikuwa safarini kikazi akitoa
huduma kwa waumini wengine.
Mama Pinda alisema alilazimika kufika kuwapa pole kwa vile alikuwa
amewasili mkoani Arusha kwa shughuli ya kikazi. “Wote tumepokea kwa
mshtuko taarifa za ulipuliwaji wa bomu pale Olasiti kwa sababu
Watanzania hatujazoea mambo ya mabomu. Tunapaswa wote kwa umoja wetu
tumuombe Mungu ili atuepushie mabaa mengine…” alisema.
Padre Lyimo aliahidi kuzifikisha salamu za Mhe. Mama Pinda kwa
Mhashamu Askofu Mkuu Lebulu na kuahidi kuendelea kushirikiana na
Serikali hadi chanzo kamili cha tukio hilo kibainike.
Aliwasihi Watanzania kuendelea kuwa na moyo wa kupendana na
kushirikiana kwa sababu wote ni wapitaji. “Sote tuko duniani, sote ni
wapitaji. Tupendane na tuombeane,” alisema.
Baadaye Mama Pinda alizuru Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia
teule ya Olasiti na kupata maelezo kamili kuhusu tukio hilo. Pia alitoa
heshima kwa marehemu watatu waliozikwa kwenye uwanja wa kanisa hilo.
Akitoa maelezo hayo mbele ya Mama Pinda, Paroko wa Kanisa hilo, Padre
Peddy Castellino alisema ujenzi wa kanisa hilo ulichukua zaidi ya miaka
sita kwa kutumia michango ya waumini wenyewe na wala hawakuwahi kupata
msaada wowote kutoka nje.
Alisema wao kama kanisa wataendelea kuomba ili tukio hilo liwe la
kwanza na la mwisho. “Tunazidi kuomba ili tukio hili lisijirudie tena
hapa nchini, na pia tunaendelea kumuomba Mungu ili waliohusika na uovu
huu waweze kukamatwa, tunataka kuona mizizi ya matukio haya iking’olewa
kabisa na matukio kama haya yasijirudie tena,” alisema.
Alimshukuru Mhe. Mama Tunu Pinda kwa kuwatembelea na kuwafariji na
kuongeza kwamba: “Tutaendelea kutetea amani katika nchi yetu ili tunu
yetu ya amani isipotee.”
Wakati huohuo, Mama Pinda leo asubuhi amewatembelea majeruhi
waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini
Arusha na kuelezwa kwamba kwenye hospitali hiyo wamebakia wagonjwa 18 na
wengine wawili wako katika hospitali ya Elizabeth wakiendelea na
matibabu. Wagonjwa wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
tangu Mei 8, mwaka huu.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Mount Meru, Dk. Josiah Mlay alimweleza Mama Pinda kwamba wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri.
Watu 66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu wamefariki dunia
Short URL: http://www.thehabari.com/?p=32849
No comments:
Post a Comment