RPC Mbeya Diwani Athuman
Na Esther Macha, Mbeya
WANAFUNZI kumi na tano(15) katika shule ya
sekondari ya Wazazi ya Lupata Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya wanashikiliwa na
jeshi la polisi kwa kosa la kuchoma moto bweni la shule hiyo kutokana na
wanafunzi wenzao kusimamishwa masomo na uongozi wa shule kwa utovu
wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
,Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya Bw.Diwani Athuman alisema kuwa tukio lilitokea
mei 14 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika shule ya sekondari
Lupata.
Bw.Athuma alisema kuwa wanafunzi hao baada
ya kuona wanafunzi wenzao watatu wamesimamishwa masomo
walianza vurugu usiku na kuanza kuchoma moto bweni
moja la wanafunzi wa kiume .
Aidha Kamanda Athuma aliwataja wanafunzi
waliosimamishwa kwa utovu wa nidhamu shuleni hapo kuwa
ni ,Joseph Robert (18) Kidato cha nne Mkazi wa Kitunda Jijini Dar es
Salaam,Mwita Chacha(17),Mwanafunzi wa kidato cha tatu
mkazi wa Jijini Dar es Salaam ,pamoja na Daniel
David(18)kidato cha Tatu mkazi wa Ipinda Kyela.
“Hawa wanafunzi watatu waliosimamishwa
masomo walihamasisha wenzao kuunga mkono kupinga adhabu hiyo kwa
kufanya vurugu na kuchoma bweni hilo la wanafunzi”alisema Kamanda
Athuman.
Alisema kuwa bweni lilochomwa
moto walikuwa wanaishi wanafunzi ambao hawakuwa tayari kuunga
mkono uvunjifu huo wa amani shuleni hapo.
Aidha Bw. Athuman alisema kuwa
kufuatia vurugu hizo vinara wawili wa vurugu hizio wanashikiliwa
na jeshi kwa mahojiano zaidi ambao ni ,Joseph Robert , Mwita Chacha huku
watuhumiwa kumi na tano wanashikiliwa na jeshi hilo.
Kuhusu
vitu ambavyo vimeharibiwa Kamanda huyo alisema thamani halisi ya uharibifu
uliotokea bado kujulikana na kwamba hakuna madhara yeyote ya kibinadamu
yaliyotokea .
Hata hivyo Bw.Athuman ametoa wito kwa
jamii hasa wanafunzi kuacha tabia ya kujichukulia
sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake watatue
matatizo kwa njia ya meza ya mazungumzo katika mamlaka husika ili
kuepusha madhara na hasara zinazoweza kujitokeza ambazo mara nyingi
wahanga wanakuwa ni wanafunzi wenyewe.
No comments:
Post a Comment