Pages

Tuesday, May 7, 2013

Kiwia alia na fedha za EPA


 
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na sekretarieti ya chama hicho, wametakiwa wawaeleze Watanzania fedha za EPA, Richmond, Kagoda, Rada na Meremeta ziliko badala ya kufanya siasa za majitaka dhidi ya CHADEMA.
Akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika juzi viwanja vya Bugogwa Shule ya Msingi, Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), aliwataka vigogo hao wa CCM kueleza zilipo au matumizi ya fedha hizo.
Alibainisha kuwa Kinana na timu yake wanatakiwa kuueleza umma walivyohusika katika ufisadi huo pamoja na sababu za serikali ya CCM kushindwa kuwachukulia hatua mafisadi badala ya kuiandama CHADEMA kwa kuibambikia tuhuma zisizo za kweli juu ya ugaidi.
Alisema ufisadi huo umeligharimu taifa na kusababisha ongezeko kubwa la umaskini kwa Watanzania hivyo ni vema majibu ya kuridhisha yakatolewa badala CCM kufanya propaganda na siasa za hovyo.
“Huyu Kinana na timu yake nzima ya sekretarieti wanapokuja kwenu wananchi wanatakiwa waje kama watuhumiwa wa serikali yao kushindwa kudhibiti ufisadi. CCM haitaki wananchi mpate maendeleo maana mtaelimika muikatae isiwatawale.
“Wanatakiwa wawaeleze wananchi nani kachukuwa fedha za EPA, Kagoda, Meremeta, Rada na zile fedha za Richmond. Waulizeni wawaambie na sababu ya serikali yao ya CCM kwa nini imeshindwa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa ufisadi,” alisema Mbunge Kiwia kisha kushangiliwa.
Alisema CCM na serikali yake imeshindwa pia kuwakamata vigogo wanaodaiwa kuficha mamilioni ya fedha nchini Uswisi licha ya serikali ya nchi hiyo kuwa tayari kutoa ushirikiano dhidi ya mafisadi hao, jambo linalozorotesha upatikanaji wa maendeleo ya taifa na wananchi wake.
Kiwia aliwasihi wananchi kuhakikisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani waichague CHADEMA na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wafanye hivyo hivyo ili kujikomboa kutoka katika mikono ya CCM.

No comments:

Post a Comment