Pages

Wednesday, May 8, 2013

Ratiba Ligi ya Mabingwa mikoa hadharani


RATIBA ya Ligi ya Mabingwa Mikoani (RCL), ilipangwa jana, huku mabingwa wa mikoa ya Dar es Salaam (Red Coast), Lindi (Kariakoo) na Kigoma (Saigoni) wakianzia nyumbani katika mchakamchaka huo unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 11-12.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, ligi hiyo itachezwa kwa mtoano wa nyumbani na ugenini ambapo mwenyeji atapanga tarehe ya mechi ambazo zinatakiwa kuchezwa kati ya Jumamosi au Jumapili, huku marudiano ya raundi hiyo ya kwanza yakipamgwa kuchezwa kati ya Mei 18 na 19.

Zoezi la upangaji ratiba ya michuano hiyo ulishuhudiwa na waandishi wa habari kwa niaba ya klabu husika ambapo mabingwa wa mkoa wa Shinyanga (Stand Ngaya FC) wamepita moja kwa moja hadi raundi ya pili itakayochezwa kati ya Mei 25 na 26 na kurudiana Juni 1 na 2.

Raundi ya tatu itachezwa kati ya Juni 8 na 9, wakati marudiano ni Juni 15 au 16 mwaka huu, na raundi ya nne itachezwa kati ya Juni 22 au 23 na marudiano ni Juni 29 au 30. Raundi ya tano ni kati ya Julai 6 na 7, na marudiano ni Julai 13 au 14.

Timu mbili za kwanza zitapanda moja kwa moja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao, wakati timu ya tatu itapatikana kwa timu zilizoshindwa hatua ya nusu fainali kucheza zenyewe kwa zenyewe.

Washindi wa nusu fainali nao watacheza wenyewe kwa wenyewe ili kupata bingwa wa RCL ambaye atakabidhiwa kombe la ubingwa.

Ligi hiyo inashirikisha mabingwa kutoka mikoa 27 ya kisoka, ambapo katika raundi ya kwanza wanaanza mabingwa 26, raundi ya pili ni mabingwa 14 wakijumuisha na bingwa wa Shinyanga ambaye ameingia moja kwa moja katika hatua hiyo.

Raundi ya tatu itashirikisha timu saba zilizosonga mbele pamoja na moja yenye uwiano mzuri wa matokeo ili kufanya jumla ya timu nane, raundi ya nne itakuwa na timu nne wakati raundi ya tano itakuwa ni kumpata bingwa na mshindi wa tatu.

Katika upangaji huo wa ratiba mechi za raundi ya kwanza itakuwa kama ifuatavyo: Red Coast itawakaribisha Abajalo, Kariakoo itakuwa nyumbani kuwakaribisha Mtwara, huku Friends Rangers ikiumana na Kiluvya United.

Teckfolt FC itakuwa dimba la nyumbani kuwaalika African Sports, huku Machava FC ikipimana ubavu na Flamingo SC, Gunners United itacheza na Manyara nayo Simiyu ikipigana vikumbo na Magic Pressure FC.

Mechi nyingine, Polisi Jamii Bunda FC itakuwa na kibarua mbele ya UDC FC, wakati Geita itacheza na Biharamulo SC, huku Saigoni SC ikitoana jasho na Tabora. Katavi Warriors itaonyeshana kazi na jirani zao Rukwa United, huku Mji Njombe ikiwa nyumbani kuwakaribisha Mbinga United na Kimondo FC itafunga kazi na Iringa.

Aidha taarifa ya Wambura imesisitiza kuwa mechi zote za RCL zitachezwa katika viwanja vya makao makuu ya mikoa, labda zile ambazo zitakuwa na maombi rasmi ambayo yatapitiwa na kupata ridhaa ya TFF.


No comments:

Post a Comment