Pages

Thursday, May 9, 2013

Sitta ainusuru Bajeti ya Wizara ya Nchimbi

 

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta juzi aliinusuru Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kujibu kwa hekima hoja ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyekuwa ameamua kutoa shilingi.                

Lissu alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi baada ya kuleta hoja ya kutaka Jeshi la Polisi lifanyiwe marekebisho.

Pia alieleza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya, wanatumia jeshi hilo kuwazuia wapinzani kufanya mikutano, madai aliyosema yanasababisha vurugu na kupandikiza chuki.

Mbunge huyo machachari  alieleza kuwa ripoti ya Jaji Steven Ihema iliyoteuliwa na Waziri Nchimbi kuchunguza kifo cha Mwandishi wa Habari wa Televisheni ya Channel Ten Daudi Mwangosi ilieleza kuwa Polisi inatakiwa kupanguliwa kutokana na kupendelea upande mmoja.                

Pia alikariri ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu ya Serikali iliyotuhumu kuwa polisi inaipendelea CCM na kuvionea vyama vya upinzani.

Mapema Nchimbi akijibu hoja hiyo kwa kudai wale wote, ambao wanaishia kiujanja ujanja na kulikosea jeshi hilo ndiyo wanaolalamika tofauti na wale waliopata msaada wa jeshi na hasa katika kipindi cha ajali wanaliona likifanya kazi nzuri.

Hata hivyo Lissu hakufurahishwa na jibu hilo kwa madai ni jepesi na ndipo Sitta kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alimpoza kwa kueleza hoja yake ilikuwa na uzito lakini inahitaji muda mrefu wa kujadiliwa.

“Nadhani hapa si mahali pake. Hizi ni tuhuma nzito dhidi ya polisi na CCM zinazotolewa na upinzani. Ninamwomba mheshimiwa Lissu aandae hoja binafsi halafu ije ijadiliwe kwenye kikao kijacho”alishauri Sitta na ombi lake lilikubaliwa na Lissu.

Mapema Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango,Kangi Ligola (Mwibara-CCM) na Felix Mkosamali (Kibongo-NCCR-Mageuzi) nao walitaka maelezo ya kina kutoka kwa waziri huyo juu ya suala hilo.

Kiasi cha Sh741 bilioni zilipitishwa jana bungeni kama bajeti ya wizara hiyo huku fedha nyingi zikipunguzwa kutoka katika maeneo mengine kutokana na kuanzishwa kwa mikoa mipya.

 

Source Mwananchi.

No comments:

Post a Comment