Pages

Thursday, May 9, 2013

Tendwa: Siyo kila kinachosemwa upinzani ni kibaya

 


Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa 

Ikiwa imebaki miezi miwili Tanzania itimize miaka 21 tangu iingie katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema hoja nyingine zinazotolewa na vyama vya upinzani ni za msingi na zinatakiwa kufanyiwa kazi.
Amesema katika kipindi cha miaka 21, vyama vya upinzani vimeimarika na viongozi wake wametoa hoja za msingi kwa maendeleo ya taifa, huku akisisitiza kuwa kama vikisema ukweli unatakiwa kufanyiwa kazi na siyo kubezwa.

Mfumo wa chama kimoja ulidumu kwa miaka 27 (1961-1992), ulibadilishwa ili kuurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa kutokana na marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria namba 5 ya mwaka 1992.

Akizungumza  ofisini kwake , Tendwa alisema demokrasia imekuwa kwa kiwango kikubwa na kutolea mfano mvutano kati ya CCM na Chadema, akisema kuwa unatakiwa kuchukuliwa kama mgongano wa kisiasa na si vinginevyo.

“Kikubwa ambacho viongozi wa chama tawala na wale wa upinzani wanatakiwa kujihadhari nacho ni lugha za matusi na kujihusisha na mambo ambayo yanaweza kuleta uvunjifu wa amani,” alisema Tendwa na kuongeza;
“Pamoja na mivutano iliyopo ukweli unabaki palepale kwamba vyama vipo vingi na vyote haviwezi kuibuka na ushindi.”

Alisema hata nchini Marekani, Chama cha Republican na Democratic vina upinzani mkali na wakati mwingine viongozi wake hurushiana maneno ya hapa na pale, “hiyo ndiyo siasa ya vyama vingi.”

Alisema asilimia 80 ya kazi ya siasa ni propaganda na alisisitiza kuwa yanayozungumzwa na wapinzani yanalenga kuwaeleza Watanzania kuwa CCM haijafanya lolote.

Source :Mwananchi

No comments:

Post a Comment