Wauguzi waonywa matumizi ya simu
WAUGUZI nchini wameshauriwa kuacha simu zao katika vyumba maalumu au kuzizima wakati wanapotoa huduma kwa wagonjwa.
Wito huo ulitolewa juzi na muuguzi mstaafu Andulile Mwansyange (68)
alipokuwa akitoa tofauti ya utumishi wake na uuguzi wa sasa katika
maadhimisho ya Siku ya Uuguzi Tanzania iliyofanyika Mbalizi-Ifisi,
Mbeya.
Mwansyange alisema mjadala unahitajika kuhusu umuhimu wa wauguzi kutotumia simu za viganjani wakiwa kazini.
“Kuwe na mjadala wa wauguzi kutotumia simu wanapokuwa kwenye vyumba
vya kutolea huduma muhimu pia wagonjwa wafunge simu wanapoingia kwenye
matibabu.
…Unaweza kupigiwa simu ya msiba au kupokea ujumbe wa mtu anayekuhusu
hali inayoweza kusababisha kuacha kutoa huduma kwa mgonjwa,’’ alisema
muuguzi huyo mstaafu.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Upendo Sanga, alisema
angekuwa mkufunzi wa wauguzi angewafundisha maadili na watakaoshindwa
angewafukuza uuguzi.
Akisoma risala kwa niaba ya mkurugenzi huyo aliyekuwa mgeni rasmi,
mwanasheria wa wilaya hiyo, Prosper Msivala, alisema suala la matumizi
ya simu kwenye maeneo ya kutolea huduma limekatazwa na lipo kisheria
hivyo halihitaji mjadala.
Naye Muuguzi Mkuu wa hospitali ya Mbalizi Ifisi inayomilikiwa na
kanisa la Uinjilisti Tanzania, Sikitu Mbilinyi, alisema upendo kwa
wagonjwa ni tiba, hivyo umefika wakati kwa kila muuguzi kubadilika.
No comments:
Post a Comment