Aliyetenda uovu anaweza kujitakasa mbele ya jamii?
“Nilipata mimba shuleni, wazazi wangu walikasirika sana, wakanisusa.
Tangu hapo nimekuwa nikiwaambia nataka kusoma, wanasema hawawezi
kumsomesha mhuni.”
Msichana mmoja alinisimulia kisa hiki hivi karibuni.
Baada ya simulizi hii nzito nilimtazama yule msichana kwa huruma.
Nikamuuliza kama aliwaomba msamaha wazazi wake baada ya kosa lile?
Alinijibu: “Niliwaomba lakini hawajanisamehe.”
Yawezekana nawe msomaji wangu unapoungana nami kwenye mada hii ni
miongoni mwa watu waliotengwa na jamii kwa sababu ya makosa yako.
Maisha yako ya nyuma yalikuwa ya wizi na ujambazi kiasi cha kuwafanya
hata ndugu zako wakutilia shaka unapowatembelea.
Inawezekana ulikuwa kahaba, mkabaji, mtumia dawa za kulevya, mhuni ila
kwa sasa umeachana na uovu wa aina hiyo lakini tatizo limebaki kwa jamii
kuendelea kukuweka katika tabia ulizoachana nazo.
Miaka kumi imepita tangu umeacha wizi lakini bado huaminiki, umebaki
kujiuliza kwa nini jamii haikusamehe? Inakuwaje watu wanashindwa
kubadilika sawa na uamuzi wako wa kuachana na ukahaba na badala yake
wamebaki na picha ile ile ya maisha yako ya zamani?
Katika hali ya kawaida, si rahisi jamii kusahau uhalifu wako na hasa
kama wewe mwenyewe hujafahamu namna ya kusafisha madoa ya uchafu wako.
Niko kwenye ukurasa huu kwa ajili ya kukushauri mambo ya kufanya ili
uweze kujitakasa. Umfanye baba aliyekasirika baada ya kupata ujauzito
akuamini tena. Umrejeshee imani bibi yako uliyemuibia miaka sita
iliyopita akuchukulie tofauti na mwanzo. Angali dokezo zifuatazo.
KUKIRI MAKOSA
Watu wengi wanaponya uovu huwa wanaamini kuwa, wakiacha uovu fulani
jamii itawaelewa na kuwasamehe moja kwa moja na hivyo kutoona umuhimu wa
kukiri makosa mbele ya jamii, kitu ambacho si sahihi.
Ukweli ni kwamba, kama umekuwa mkosaji wa hili na lile hakikisha
unapoachana na tabia hiyo unarudi kwenye jamii au mtu uliyemkosea na
kumuomba msamaha.
Mwambie akusamehe kwa uovu wako na kumwahidi kutorudia tena, usikae
kimya na kudhani atakusamehe hivi hivi tu. Anza kuishi maisha mapya
yaliyo mbali na makosa.
TANGAZA MABADILIKO
Wakati unakusudia kuachana na uovu fulani uliokuwa ukiutenda, watangazie
watu wakiwemo rafiki zako kuwa unabadilika kutoka kwenye tabia mbaya na
kuishi maisha mema.
Ukiacha bila kutangaza ni rahisi watu kudhani
umepumzika tu kwa muda kuiba na kwamba siku zijazo utarudia hivyo
kutokukuamini.
TUMIKIA WEMA
Sote tunajua matendo ndiyo yanayoweza kutafsiri tabia ya mtu kwa urahisi
zaidi kuliko kitu kingine.
Wengi huitwa malaya kwa sababu wanafanya
vitendo vya ukahaba, wanaiba ndiyo maana wanaitwa wezi.
Ukisema umeacha uhuni lazima ukate mizizi yote itakayokuhusisha na tabia
hiyo na kutumikia uaminifu kwa vitendo.
Ukifanya hivyo, baada ya muda
jamii itakusamehe na kubaki na historia ya: “Alikuwa mhuni lakini
amebadilika, enzi zake alikuwa mwizi, siku hizi ameacha. Asante!
No comments:
Post a Comment