CHADEMA yaishtukia CCM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kimebaini mbinu chafu na njama zinazotumiwa na CCM kuvuruga chaguzi ndogo za kuziba nafasi za madiwani kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Njama hizo zimefichuliwa kutokana na taarifa za ndani walizozipata za kuwepo kwa maagizo maalumu kutoka kwa viongozi wa chama hicho yanayowaelekeza mabalozi wa nyumba kumi kumi wa CCM kuhakikisha kuwa kila balozi anafanikiwa kununua shahada zisizopungua kumi kutoka kwa watu waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Sambamba na agizo hilo, uchunguzi uliofanywa na viongozi wa CHADEMA wanaeleza kuwa wamegundua kuwepo kwa mbinu chafu za kughushi shahada za kupigia kura kwa kukusanya kutoka kwa ndugu za wapiga kura waliokufa na kuzibadilisha ili zitumike katika chaguzi hizo.
Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija na msimamizi wa operesheni ya ushindi wa chama hicho kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alisema jana kuwa utafiti walioufanya wamebaini kuwepo kwa vitendo viovu vya kuvuruga chaguzi hizo vinavyofanywa na CCM kwenye kata zinazotakiwa kuwachagua madiwani wapya.
Mwambigija alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa CCM wanashinda kwenye Kata ya Iyela jijini Mbeya ambayo diwani wake, Dominick Tweve (Mzee Nkwenzulu) alifariki dunia, kundi la vijana wa chama hicho wameweka kambi na kupatiwa mafunzo maalumu ya kuvuruga uchaguzi ambao kampeni zake zinatakiwa kuanza Mei 15, mwaka huu.
Alisema kuwa vijana wa CCM wameweka kambi eneo la Mwangonela jirani na kilipokuwa chuo cha ufundi cha Jakaranda na wamekuwa wakishirikiana na mabalozi wa nyumba kumi wa chama hicho kukusanya na kupatiwa shahada za wapiga kura waliokufa ili ziweze kughushiwa kwa lengo la kutumiwa kwenye uchaguzi huo.
“Napenda kukuthibitishia kuwepo kwa njama hizo, CHADEMA tunawaomba wenzetu CCM wakubali kufanya uchaguzi huru na wa haki bila kutumia mbinu chafu au polisi, tutumie demokrasia ili chaguzi hizi ziwe na amani, watu wapige kura bila kununuliwa na waache kukusanya shahada za wapiga kura, huo ndio wito wangu,” alisema Mwambigija.
Alisema kuwa kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani, Kata ya Myovizi, Wilaya ya Mbozi walibaini wananchi waliopewa shahada za kughushi na walipogundulika walikimbia na baadhi ya shahada walizozikamata waliziwasilisha polisi kama ushahidi.
Chanzo :Chadema blog.
No comments:
Post a Comment