| KATIKA 
hali isiyokuwa ya kawaida, Uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mpolo kata ya 
Utengule Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya imegeuza matumizi ya Zahanati ya Kijiji 
kuwa Ofisi.
 
             Hilo 
limebainika baada ya Waandishi wa Habari kutembelea eneo hilo na kukuta majengo 
ya Zahanati hiyo yakitumika kama Ofisa ya Mtendaji wa Kijiji, Ofisi ya 
Mwenyekiti na Ofisi kwa ajili ya Baraza la Usuluhishi la 
Kijiji. 
Mwenyekiti 
wa Kijiji hicho Andres Mlongosi,  alipohojiwa kuhusiana na tuhuma za kugeuza 
matumizi ya Jengo ambalo lilitakiwa litumike kwa ajili ya Zahanati lakini wao 
wanalitumia kama ofisi alikiri kufanya kinyume kwa kile alichodai Serikali ya 
Kijiji haina ofisi kutokana na jengo lilikuwa likitumika awali 
kubomoka. 
Aliongeza 
kuwa wako kwenye mpango wa kujenga upya ofisi yao ambapo baada ya kukamilika 
Jengo hilo litaachwa litumike kama ilivyokuwa imekusudiwa kwa matumizi ya 
Zahanati ambapo hadi sasa Wananchi hupata matibabu katika Kituo cha Afya cha 
Utengule, Igurusi au Hospitali ya Misheni ya Chimala sehemu ambazo ni 
mbali. 
Aidha 
wananchi hao wameendelea kupata adha ya matibabu hasa Wanawake wajawazito ambao 
hutumia muda mrefu kusafiri kufuata matibabu pamoja na Wazee wasiojiweza ambapo 
hutembea kwa zaidi ya Kilomita 15. 
Kwa 
upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Utengule, Benyanga Zuberi amethibitisha 
uwepo wa hali hiyo na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali  ndiyo 
iliyosababisha hali hiyo kutokana na kutotuma fedha za kumalizia maeneo 
yaliyobaki kama Choo. 
Alisema 
suala la kuweka Ofisi kwenye majengo ya Zahanati ni suala la Mpito ambapo baada 
ya kukamilika kwa ujenzi kwa asilimia zote Zahanati itaendelea kama kawaida 
hivyo Wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu hali hiyo. 
Nao 
Wananchi wa Kijiji hicho walisema wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa na 
uongozi wa Kijiji cha kugeuza majengo ya Zahanati kuwa ofisi licha ya kutumia 
nguvu nyingi kuchangia ujenzi huo. 
Walisema 
kitendo hicho si cha uungwana na kinakatisha tamaa wananchi kuendelea kujitolea 
nguvu na michango katika kufanikisha ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo 
kama wataendelea kugeuza matumizi tofauti na inavyokuwa 
imekusudiwa. 
Diwani 
wa kata ya Utengule Juntwa Mwalyaje alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba 
Baraza la dharula lililoketi Mei 6, Mwaka huu lilikutana kujadili mustakabali wa 
zahanati hiyo ambapo walimwomba mganga Mkuu wa Wilaya kuandika barua ya maombi 
ya fedha za kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo ikiwemu ujenzi wa Choo na Nyumba 
ya Mganga. 
Kwa 
upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Venance Gwaza Mwashala amesema 
Halamashauri ilishapitisha Shilingi Milioni Tano kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya 
Kwanza ambazo zitaingizwa katika akaunti ya Kijiji wakati wowote kuanzia 
sasa 
Aidha 
ameutaka uongozi wa kijiji kuongeza nguvu zao ili waweze kukamilisha mapema 
ujenzi huo na kuletewa waganga na huduma zote ili kupunguza adha kwa wananchi ya 
kufuata matibabu mbali. | 
No comments:
Post a Comment