Pages

Thursday, May 9, 2013

Daktari kortini akidaiwa kughushi nyaraka NHIF

DAKTARI wa Hospitali ya Aga Khan jijini Mbeya, Mashika Elineza Mashika na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakikabiliwa na makosa zaidi ya 200 ya kughushi nyaraka za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kujipatia mali kwa udanganyifu.

Washitakiwa wengine wametajwa kuwa ni Ali Hassan Kinjimbi na Muuguzi Advera Haule anayekabiliwa na makosa saba.

Mbele ya Hakimu Gilbert Ndeuruo, Mwendesha Mashitaka wa serikali Achiros Mlisa, alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo kinyume cha vifungu mbalimbali vya sheria.

Alidai Dk. Mashika alisambaza nyaraka za mfuko huo zilizogushiwa na kusainiwa na mganga asiyejulikana wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kugongwa mhuri wa hospitali hiyo.

“Dk. Mashika ulihusika kusambaza nyaraka hizo na kudai fedha katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya iliali anajua kuwa ni uongo na kujipatia mali kwa udanganyifu kwa kuchukua dawa katika maduka mbalimbali,” alidai Mwendesha Mashitaka huyo.

Hata hivyo, washitakiwa wote walikana mashitaka yao na kupewa dhamana.

Washitakiwa hao leo wanatarajiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment