Pages

Tuesday, May 14, 2013

Facebook, mitandao ya kijamii huathiri watu kisaikolojia

 

 Facebook, mitandao mingine ya kijamii pamoja na huduma ya ‘blackberry mesenger’ maarufu kama BBM huathiri watu kisaikolojia, husababisha ndoa kuvunjika pamoja na usaliti katika uhusiano, wanasayansi wamebaini.

Utafiti huo uliofanywa mwaka 2012 na wanasayansi wa nchini Israel umebaini kuwa kwa wastani, wanawake wanatumia dakika 81 katika mitandao ya kijamii kwa siku ukilinganisha na wanaume ambao hutumia dakika 64, huku watu wasio na elimu wakionekana kuathirika zaidi na mitandao hiyo.

Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Tel Aviv walihusisha matukio kadhaa ya kisaikolojia kati ya watu walioathirika na mtandao na udanganyifu uliosababishwa na uhusiano unayoanzishwa kupitia mitandao ya kijamii.

Utafiti huo ulibaini kuwa wote waliohusishwa walikuwa na tatizo la upweke, ingawa hakuna aliyekuwa na historia ya matumizi ya dawa za kulevya au matatizo ya kisaikolojia.

Watu wenye upweke walionekana kupendelea kutafuta uhusiano kupitia mitandao, jambo linaloelezwa kusababisha kuwaumiza watu hao na kuhisi kusalitiwa.

Kiongozi wa utafiti huo Dk Uri Nitzan kutoka Chuo Kikuu cha Sackler mchepuo wa Tiba na Afya ya Akili, Shalvata Mental Health Care Centre alisema: “Kama ilivyo matumizi ya mtandao yanazidi kuwa makubwa. Vivyo hivyo inavyozidi kuhusiana na masuala ya saikolojia. Mawasiliano ya kompyuta kama Facebook na makundi ya mawasiliano yaliyopo ndani ni sehemu muhimu ya habari hii.”

Utafiti huo awali ulihusisha wagonjwa watatu ambapo Dk Nitzan anasema kuwa utafiti wao ulibaini kuwapo na mawasiliano kati ya saikolojia za wagonjwa hao na mawasiliano ya mitandao ikiwemo Facebook. Dk Nitzan anasema kuwa wagonjwa wote watatu waliachana na maisha ya upweke na kupata furaha baada ya kupata wapenzi wapya kupitia mitandao.

Anasema: “Ingawa uhusiano wau huwa na mtazamo chanya awali, lakini huishia kuwa na mawazo ya kuumizwa, kusalitiwa na uvamizi wa faragha. Watu hawa walibadilishana mawazo, ikiwamo upweke na mazingira magumu katika hasira au kutengana na watu waliowapenda awali, kutokana na teknolojia hawakuwa na historia ya kunyanyaswa,” anasema na kuongeza:

“Katika kila kesi, kulikuwa na uhusiano baina ya kuwapo na maendeleo ya taratibu na ongezeko la dalili za kuathirika kisaikolojia, pamoja na udanganyifu, wasiwasi, kuchanganyikiwa na matumizi yaliyozidi ya mawasiliano ya kompyuta.

”Dk Nitzan anasema kuwa tatizo kubwa la mitandao ni watu kuanzisha uhusiano kabla ya kuonana ana kwa ana, tatizo ambalo husababisha mtu kumwona mwenzake anamfaa, huku hali ikiwa ni tofauti pindi wawili hao wanapokutana. Aliongeza kuwa wataalamu wa afya ya akili lazima waache ushawishi wa matumizi ya mitandao ya kijamii wanapozungumza na wagonjwa.

“Unapowauliza watu kuhusu maisha yao ya kijamii ni busara zaidi kuwauliza juu ya matumizi ya Facebook na mitandao mingine ya kijamii, kama matumizi ya mitandao,”anasema.

Anaongeza: “Utafiti wetu unaonyesha, wakati teknolojia kama Facebook ikiwa na faida nyingi, baadhi ya watu wamekuwa wakiathirika na mitandao hii ya kijamii, huku ikiwavutia walio wapweke au walio katika mazingira magumu katika maisha yao ya kila siku, wakati wengine wakilazimisha tabia zisizo zao.”



No comments:

Post a Comment