RUGE: Niko tayari kukutanishwa na Jaydee
MKURUGENZI wa Kampuni ya Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema yu tayari kukutana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla aliyejitolea kuleta suluhu kati yake na nyota wa kike wa Bongo Fleva, Judith Wambura 'Lady Jaydee', limeandika gazeti la Mtanzania.
Mutahaba ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu Waziri Makalla atamke kuwa yu tayari kuingilia kati mvutano uliopo baina ya msanii huyo na Ruge kwa kuwaita kuzungumza nao kwa maslahi ya wahusika na tasnia ya muziki nchini.
“Mimi kana nilivyosema katika tamko langu wiki iliyopita, kwamba niko tayari tuitwe na watu watusikilize pande zote mbili, hasa mlalamikaji na ukweli uweze kuwa wazi zaidi kwa sababu hadi sasa Lady Jaydee amezungumza mengi,” alisema.
Wakati huohuo, Ruge ameongeza kwamba tayari ameshachukua taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungua jalada polisi la malalamiko ya kutukanwa na Lady Jaydee.
“Lakini ninaweza kusema jambo hili linaweza kuzungumzika nje ya vyombo vya sheria kwani sisi tunaliona ni dogo na la mzaha, lakini lina athari kubwa katika jamii inayotuzunguka,” anasema Ruge.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Lady Jaydee aliamua kuibuka na kuituhumu Clouds Media Group kwa kutumia mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na blog yake kuwa inamuhujumu kimuziki, kuzuia matangazo ya mgahawa wake wa Nyumbani Lounge na kipaji chake kwa ujumla, tuhuma ambazo Ruge na Clouds wanazikanusha vikali.
No comments:
Post a Comment