Pages

Thursday, May 9, 2013

Yatima, watoto walio katika mazingira magumu na mtazamo wa jamii

                                  
             

Kwa kadri gonjwa la Ukimwi linavyoendelea kupukutisha watu na kuzalisha yatima wengi zaidi, kunahitajika mikakati endelevu ya kupunguza umasikini katika ngazi ya familia na yatima kuthamini kwa dhati badala ya baadhi ya watu au taasisi kuwafanya kuwa miradi ya kujinufaisha binafsi.

Tangu dunia ilipoumbwa na binadamu kuishi katika dunia hiyo, wamekuwepo watoto yatima.

Yatima hao walipatikana kwa sababu ya vifo vya wazazi wao vilivyotokana na ajali za kushambuliwa na wanyama wakali, vita vya wenyewe kwa wenyewe na magonjwa yaliyokosa tiba sahihi wakati huo. Hata hivyo, idadi ya yatima katika nyakati hizo za dunia ya awali, ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

Halikadhalika malezi ya yatima kwa familia yalikuwa yameandaliwa utaratibu maalum ambao haikuonekana kama ni mzigo mkubwa ikilinganishwa na hali ya sasa.Nyakati hizo, watoto walikuwa watoto hasa wa familia. Walilelewa kwa upendo na kuthaminiwa hasa.

Ugonjwa wa Ukimwi unaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la yatima. takwimu zinabainisha kuwa duniani kote zaidi ya watu milioni 60 wameambukizwa virusi vya ukimwi.

Ukimwi/Virusi vya Ukimwi kwa sasa ndio sababu kubwa ya vifo vya watu wengi katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara,Tanzania ikiwa mojawapo.

Idadi ya watoto wa Afrika ambao ni yatima waliopoteza mzazi mmoja au wazazi wote wawili kutokana na gonjwa hili kufikia mwaka 2001 ni milioni 12.1.Ilitarajiwa kuongezeka maradufu.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa katika utafiti wa viashiria vya Ukimwi 2003-4, asilimia 11 ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 wamefiwa na mzazi mmoja au wote wawili kutokana na kuugua magonjwa yanahusiana na Ukimwi.

Tishio la Ukimwi bado ni kubwa sana nchini ambapo uzalishaji wa yatima utaendelea kama hazitachukuliwa hatua za makusudi za kudhibiti maambukizi mapya. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, hadi sasa tiba ya ugonjwa huo haijapatikana.

Mtu anayeugua ugonjwa huu yupo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha yake. Dawa za kurefusha maisha ARVs sio tiba ya Ukimwi.

Kutokana na hali halisi ya umaskini katika familia nyingi ni kwamba mtafuta riziki anapougua Ukimwi na jitihada za kujaribu kutafuta tiba, mara nyingi husababisha kukwangua akiba yote ya mali ya familia iwe kujaribu kupata tiba ya hospitali, za asili au tiba mbadala bila ya mafanikio ya kujinusuru kimaisha.

Wzazi wanapofariki huwaacha watoto wao katika lindi la umasikini zaidi.

Katika mtindo wa maisha ya sasa ,watoto yatima wanajikuta ndio walezi wa familia wakiwa na mzigo mkubwa wa kutafuta chakula cha kujikimu, mavazi, maji, kuni na mahitaji mengine muhimu ya kimaisha.

Wilaya ya Makete mkoani Iringa ni miongoni mwa wilaya zenye yatima wengi kutokana na wazazi wao kufa kwa magonjwa nyemelezi yanayotokana na Ukimwi.

Baadhi ya watu wanatambua umuhimu wa kuwahurumia yatima.

Hata hivyo kulemewa na umasikini ukiwemo mzigo wa yatima katika familia zao, wanajikuta wanauvua ubinadamu wao na kubaki kuwatazama kwa macho tu.

Wasamaria wema wanaojitokeza kuwasaidia mara nyingi ni wa muda tu na wakati mwingine inakuwa sio endelevu au haizingatii vipaumbele.

Kuna taarifa kuwa baadhi ya wasamaria wema hao, wamekuwa wakiwatumia yatima kama vitega uchumi.

Baadhi ya wananchi wilayani Makete wamelalamikia baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali, kukusanya fedha kwa kisingizio cha kuwasaidia watoto yatima na waathirika wa Ukimwi. Hata hivyo, misaada mingi imekuwa haiwafikii walengwa.

Mchungaji Izack Chengula wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Makete, alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakiwatumia yatima kama vitega uchumi.

Kama hiyo haitoshi, baadhi ya watu kwa kutambua dhiki walizonazo yatima hao, hasa wasichana wadogo wamekuwa wakiwashawishi kufanya nao ngono.

Dhiki, utoto na ukosefu wa elimu sahihi ya kujitambua hujikuta wakilazimika kufanya ngono wakati mwingine bila ya kutumia kinga au tahadhari zozote.

Hatua hiyo inachangia kuwaweka katika hatari ya kuugua magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi.

Kundi jingine la yatima limekuwa likitumiwa kama watumishi wa ndani kwa malipo duni.

Kuna taarifa pia kuwa wanaume wa familia husika wamekuwa wakiwadhalilisha kijinsia na kuwabaka hata kuwapa mimba na kuwatekeleza.

Yatima wavulana wamejikuta wakitumbukia kufanya kazi za hatari au katika mazingira magumu ikiwemo kubeba mizigo mizito, kufanya kazi mashambani ikiwa pamoja na kunyunyiza dawa za kuulia wadudu mashambani bila ya kutumia kinga, kutumiwa kwenye machimbo ya migodi mbalimbali, kuzagaa mitaani huku wakilala popote na wakati mwingine kutumiwa kusafirisha dawa za kulevya, wizi na shughuli nyingine za hatari.

Utumikishwaji wa watoto katika kazi za hatari licha ya watoto yatima, ni pamoja na watoto kutoka kwenye familia zilizokithiri umaskini katika ngazi ya familia.

Serikali imeliweka suala hilo katika Mkakati wa Kupiga Vita Umaskini na Kuinua Uchumi (MKUKUTA) kama agenda muhimu katika kuliondoa tatizo hilo.

Tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yakiwemo yasiyokuwa ya kiserikali, yamekuwa yakifanya kazi nzuri ya kuielimisha jamii kuhusu janga hili.

Yawezekana hadi sasa ni Watanzania wachache ambao hawajasikia kuhusu janga hili, namna linavyoambukiza na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa ili kujinusuru hata kupunguza maambukizo mapya, vifo na uzalishaji wa yatima.

Kimsingi kinachotakiwa ni kufanya kila liwezekanalo kuzuia maambukizi mapya ya ukimwi kwa watu kujizuia kufanya ngono holela, kuwa na mpenzi mmoja aliye mwaminifu na ikishindikana kabisa kutumia kondomu kikamilifu.

Watu wawe na utamaduni wa kupima damu kwa hiyari kujua hali za afya zao ili kama wakijijua kuwa tayari wameambukizwa wajue namna ya kujitunza kwa kuzingatia ushauri nasaha, kutotapanya mali ya familia na kuwawekea msingi mzuri wa elimu kwa watoto ili watakapobaki yatima waweze kujimudu. Na ikibidi kuwaandalia mirathi.

Serikali ijenge mazingira ya kuinua hali bora za wananchi kwa dhati hasa kutoka katika lindi la umasikini uliotopea ili kuwapa unafuu yatima na watoto wasijitumbukize kuishi katika mazingira magumu.

Pia kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa wagonjwa wa Ukimwi wanasaidiwa kujikimu sio kuwapa dawa peke yake. Mkakati maalum uwalenge makundi maalum kama vile wajane,yatima na waathirika wengineo wa Ukimwi.

No comments:

Post a Comment