|
TRA
|
TRA: Tukielekezwa tutafanya uchunguzi
TBS: Tupeni muda, tutaongea jumanne
Kashfa ya ukwepaji kodi na uingizaji bidhaa
zinazosadikiwa kuwa bandia, imeibuka wakati bidhaa hizo zikipitishwa
katika `bandari bubu’ iliyopo kwenye ufukwe wa Mbweni jijini Dar es
Salaam, NIPASHE Jumapili limebaini.
Hali hiyo inayohujumu uchumi wa taifa, inafanyika huku jiji hilo
likiwa Makao Makuu ya vyombo vya dola vyenye mamlaka na majukumu
tofauti, yanayoweza kuudhibiti uovu huo.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini kuwa shehena za bidhaa
mbalimbali yakiwamo mafuta ya kula, zinaingizwa bila kificho kwenye
`bandari’ hiyo, kisha kusafirishwa maeneo tofauti ya nchi. Kwa hali hiyo, `bandari bubu’ isiyokuwa na udhibiti wa aina yoyote,
imekuwa moja ya vituo vikuu vya kukwepa kodi na uingizaji wa bidhaa
`feki’.
Licha ya hujuma hizo, bidhaa zinazopitia katika eneo zikitokea nje
ya nchi, zimekuwa kichocheo cha ‘kuua’ bidhaa za ndani, kutokana na
kutolipiwa kodi na ushuru, hivyo kuuzwa kwa bei rahisi zaidi. “Unaponunua bidhaa zilizopitishwa Mbweni, gharama yake ni ndogo
hivyo inakuwa rahisi kulimiliki soko la ndani na kuua ushindani,”
kilieleza moja ya vyanzo vyetu.
Miongoni mwa bidhaa za ndani zilizoathirika kutokana na kuwepo kwa `bandari bubu’ hiyo ni mafuta ya kula yanayozalishwa nchini. Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa, shehena za mafuta ya kula kutoka
nje, zimekuwa zikishushwa kisiwani Unguja na kuingizwa Tanzania Bara kwa
majahazi yenye uwezo wa kubeba ‘madumu’ 500, kisha kupakuliwa katika
`bandari bubu’ ya Mbweni.
Ingawa haikujulikana ikiwa waingizaji wa bidhaa hizo ni
wafanyabiashara halali ama wafanya magendo, lakini baadhi ya mafuta ya
kula ambayo nembo zake zilionekana ni Oki, Asma, Partner, Viking na
Premier Gold kutoka Malasyia. Mafuta hayo yanapofika sokoni, yanauzwa kwa kati ya Shilingi
38,0000 hadi 45,000 kwa ujazo wa lita 20, wakati bei ya mafuta ya kula
yanayotengenezwa nchini kwa ujazo huo ni kati ya Shilingi 52,000 na
55,0000.
Baadhi ya wafanyabiashara katika eneo la Mbweni, walithibitisha
kuwepo hujuma ya ununuzi wa bidhaa hizo, licha ya kuwepo msako
unaofanywa mara chache na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA). Walisema, TRA inafanya msako hadi majini, lakini kutokana na
mazingira yanayoashiria rushwa, ushushaji wa shehena hizo umekuwa
ukiendelea.
"Unajua hela ni kila kitu, TRA wanawakamata wahusika, wakipewa
hongo hawachukui hatua yoyote… wafanyabiashara wengi wanaingiza bidhaa
nyingi kupitia hapa na si mafuta ya kula tu," kilieleza chanzo hicho. Mmoja wa wafanyabiashara wa Tegeta jijini Dar es Salaam, John
Massawe, anathibitisha kuwepo bidhaa yakiwamo mafuta ya kula, zinazouzwa
kwa ‘bei chee’ kutokea Mbweni.
Anasema gharama ndogo za ununuzi wa `mafuta ya Mbweni’ zinamfanya awekeze katika kuyanunua na kuyauza, hivyo kupata faida kubwa. “Mafuta ya Tanzania yanachukua muda mrefu kutoka kwa sababu ya
ukubwa wa bei yake ikilinganishwa na haya yanayotoka nje kupitia
Mbweni,” alisema.
Zipo taarifa zinazowahusisha baadhi ya wafanyabiashara wakubwa
katika uingizaji wa bidhaa na mafuta ya kula kupitia ‘bandari bubu’
hiyo. "Kwa sasa siagizi tena haya mafuta ya ndoo kwani yana hasara,
ninanunua yanayotoka nje ya nchi kama Premier, yanauzika kwa haraka na
sijapata malalamiko kama yana madhara," alisema
WAMILIKI WA VIANYA WAJA JUU
Baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya kula,
wamelalamikia hujuma zinazofanyika kwenye bandari hiyo, kwamba
zinawasababishia hasara. Christopher Mutayoba ni mmiliki wa kiwanda cha CRM Investment,
anasema kushindwa kuidhibiti hujuma zinazofanywa kwenye ‘bandari bubu’
ya Mbweni, kunadidimiza viwanda vya wazawa na kuvifanya vishindwe kukua.
Mutayoba alisema serikali inapaswa kuchukua hatua kali zenye nia na
utashi wa kuwatetea wazawa, ili waweze kulimiliki soko la ndani na
kusafirisha bidhaa zao nje. "Ukiona tunafanya biashara ya mafuta ni mpaka yanayotoka nje yakosekane sokoni,” alisema.
Mmiliki mwingine wa kiwanda cha mafuta ya kula jijini ambaye
hakutaka jina lake liandikwe gazetini, amethibitisha bidhaa hiyo kukosa
soko la ndani. vAlisema serikali inakusanya kodi kubwa kwa viwanda vya ndani,
wakati bidhaa za nje zikiingizwa kinyemela bila kulipiwa kodi na ushuru.
Catherine John ni mkazi Kinondoni, alisema haelewi kama mafuta hayo
yana madhara, lakini amekuwa akiyanunua kutokana na kuuzwa kwa bei
rahisi. Baadhi ya vyombo vya kuhifadhiwa mafuta hayo vimebainika kuwa na
nembo ya uthibitisho ya Shirika la Viwango (TBS) huku mengi yao yakiwa
hayana.
Taarifa zinadai kuwepo ushindani mkali katika ununuzi wa mafuta
hayo, kutokana na kuhitajiwa na wafanyabiashara wengi hasa wa rejareja.
Yanapopakuliwa, mafuta hayo yanasafirishwa kwa kutumia magari binafsi na wakati mwingine daladala. NIPASHE Jumapili ilishuhudia sehemu ya shehena iliyopakiwa kwenye
daladala, ikishushwa eneo la Tegeta na kupakiwa kwenye garia aina ya
Fuso iliyokuwa imeegeshwa kandoni mwa barabara.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu wa TRA, Richard Kayombo, alisema
wanachohitaji ni kupata taarifa kamili kuhusu hujuma hiyo ili
waishughulikie. "Ni kweli kuna bandari bubu, ila tunaomba utupatie taarifa kamili
za huo mzigo ili tufahamu umeingizwaje, unamilikiwa na nani, aliyeuagiza
na unashukia eneo lipi, ili tuwapatie maafisa wetu na polisi kwa
uchunguzi," alisema
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Mahamoud Mgimwa, alisema hawana taarifa kuhusu hujuma hiyo. "Hata mimi nimeshangazwa, iweje mafuta hayo yanayotoka nje yauzwe rahisi kiasi hicho, huko nikuua viwanda vya ndani," alisema.
Mkurugenzi wa Uthibiti wa Ubora wa TBS, Tumain Mtitu, alisema hawana ‘data’ kamili na kwamba hawaijui kashfa hiyo. "Nifuate wiki ijayo kwa sasa nashindwa kuzungumzia kwa kuwa sina `data’ kamili, nitumie hayo majina ya hayo mafuta," alisema.
No comments:
Post a Comment