Profesa Sifuni Mchome
Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa
wa Kidato cha Nne mwaka 2012, imetoa mapendekezo 130, mojawapo ikitaka
kupitiwa upya kwa mitalaa ya elimu nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi
hadi vyuo vya ualimu itazamwe upya.
Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Februari 23, mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi
kupata daraja la sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.
Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.
“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha
kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya
mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya
kumaliza mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya
kwa mitalaa yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba
kwa elimu ya msingi, minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano
na sita.
“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada
ya miaka minne tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based
competence’ (kuangalia ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari
umemaliza mzunguko wake na haya matokeo yametokana na mtalaa huu.
Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema.
Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa
njia rahisi ya kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya
kusubiri mpaka vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.
“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke
vitabu kwenye system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa mwanafunzi
atakayesoma sana atapata zawadi,” alisema na kuongeza.
“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama
Mwananchi ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi
mzima na shule ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa
Sh30,000 kwa kila shule na tatizo la vitabu litakwisha.”
Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa
sheria mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na
kuhakikisha madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment